Mgonjwa mwengine athibitika kuugua Ebola Goma Mashariki DRC
31 Julai 2019Hofu kubwa imetanda kwa mara nyingine mjini Goma mashariki mwa Kongo baada ya kutangazwa kuweko kwa mgonjwa wa pili wa homa ya Ebola huku afisa mkuu aliyeteuliwa naye Rais Felix Tsishekedi kwa ajili ya kupambana na mlipuko huu ameahidi kuanzisha operesheni ya chanjo.
Kulingana na madaktari wa afya Kivu Kaskazini wamesema kwamba mgonjwa wa Ebola alingia mjini Goma akitokea jimbo la Ituri wiki mbili zilizopita, huyo alitengwa baada tu ya kuonesha dalili zote za homa hatari ya Ebola na kupelekwa kwenye eneo maalumu ili kupewa matibabu.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Goma, kiongozi wa kikosi kinachopambana na Ebola mkoani Kivu kaskazini na Ituri Jack Muyembe ameeleza kwamba mikakati imechukuliwa ili mgonjwa huyu apokee matibabu mjini Goma.
Hata hivyo ,afisa huyu aliyeteuliwa naye rais Tshisekedi baada ya kujiuzulu kwake waziri wa zamani wa afia nchini amesema kwamba operesheni ya chanjo itaanzishwa mjini Goma kwa lengo la kuzuia maambukizi mapya kwa wakaazi wanaoonekana kuishi katika wasiwasi.
Kisa hiki cha pili kimegunduliwa mwezi mmoja baada ya mchungaji wa kanisa la wakiprotestanti kufariki kutokana na ugonjwa huo wa Ebola wakati alipokuwa akirejeshwa mjini Butembo. Ripoti ya wiki kutoka shirika la WHO imebainisha kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na Ebola imefikia 1803 na watu 770 wamepata afueni tangu mwezi wa Agosti mwaka jana.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya shirika la afya duniani WHO kutangaza kwamba homa ya Ebola ni janga la kimataifa na kutaka uungwaji mkono wa mataifa yote ili kukabiliana na ungonjwa huo hatari.