Mgomo wa kitaifa Nigeria waingia siku ya pili
10 Januari 2012Shughuli nyingi za kibiashara zilifungwa katika miji mikuu nchini humo na usafiri kutatizika licha ya maandamano ya siku ya pili yaliyoitishwa na vyama vya wafanyakazi katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos kuvutia watu wachache kufikia saa 2:30 asubuhi.
Mgomo huo umechochewa na hatua ya serikali ya kuondoa ruzuku ya mafuta kuanzia tarehe 1 Januari iliyosababisha bei ya mafuta ya petroli kuongezeka maradufu katika taifa hilo ambalo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika na ambapo wengi wa raia wake milioni 160 wanaishi chini ya dola moja kwa siku.
Genge la vijana leo limechukua fursa hiyo ya kuwepo mgomo na kuweka vizuizi barabarani kwa kuchoma magurudumu ya magari katika eneo moja mjini Lagos linaloishi watu mashuhuri na matajiri na kuitisha pesa kutoka madereva ili kuwaruhusu kutumia barabara hiyo.
Wafanyaibiashara pia katika mji huo hawakufungua maduka yao na masoko kufungwa kwa kuhofia kuwa wahalifu watawapora.
Mwanaharakati mmoja wa wafanyakazi Daniel Ejiofor amesema mgomo huo utaendelea hadi serikali itakaposikia kilio cha wananchi na kubatili hatua yake.
Hapo jana maelfu ya waandamanaji walijitokeza kuitikia wito wa vyama vya wafanyakazi wakupinga kuondolewa kwa ruzuku hiyo ambayo imeathiri bei ya bidhaa za kimsingi kutokana na bei ya mafuta kuongeza.
Wanigeria wanaona ruzuku hiyo kama faida pekee kutoka utajiri wa mafuta walio nao kama nchi inayozalisha mafuta kwa wingi barani Afria na hawana imani kwa serikali kuwa watatumia fedha hizo kuleta maendeleo baada ya miaka mingi ya kuzongwa na ufisadi.
Serikali imesema ilitumia dola bilioni 8 kwa ruzuku mwaka jana na kwamba inahitaji pesa hizo ili kuboresha miundo mbinu nchini humo ambayo iko katika hali ya kusikitisha.
Mgomo huo unawadia huku serikali ya Rais Goodluck Jonathan pia ikikumbwa na tatizo sugu la kukabiliana na kundi la kiislamu lenye msimamo mkali la Boko Haram ambalo limefanya misururu ya mashambulio hasa Kaskazini mwa taifa hilo yanayowalenga wakristo na kutikisa usalama wa taifa hilo na kuzua hofu kubwa miongoni mwa raia.
Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri: Othman Miraji