Mgombea wa urais Groth aukosoa uongozi wa DFB
12 Agosti 2019"Katika DFB, wanachojali tu ni hela nyingi, na mapambo tu. Hakuna wanaojali sana vilabu visivyo vya kulipwa,” Groth ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA katika mahojiano. "DFB imepoteza uhalali.”
Groth mpaka sasa ndiye mgombea pekee aliyejitosa ulingoni kuwania wadhifa wa urais wa DFB kuchukua mikoba ya Reinhard Grindel, aliyejiuzulu Aprili kuhusiana na kashfa ya kupokea saa ya mkononi yenye thamani kubwa, na malipo aliyopokea kutoka kwa shirika tanzu la DFB.
Mtangulizi wa Grindel, Wolfgang Niersbach, pia alijiuzulu, kuhusiana na sakata la Kombe la Dunia la 2006 lililoandaliwa nchini Ujerumani.
Groth mwenye umri wa miaka 60 anasimamia klabu ndogo ya DJK TuSA 06 Düsseldorf lakini hatarajiwi kukubaliwa na DFB kwa sababu hana uungwaji mkono wa lazima kutoka kwa shirikisho la kikanda. DFB inataka kumtangaza mgombea wa wadhifa huo baadaye mwezi huu, huku uchaguzi rasmi ukitarajiwa Septemba.
DFB ambalo ndilo shirikisho kunwa kabisa la kandanda duniani likiwa na wanachama milioni 7 halijawahi kuongozwa namwanamke katika miaka yake 119.
Groth anaamini hilo halitabadilika na wadhifa huo "utaamuliwa miongoni mwa watu hao hao 10.”
"Hicho ndicho watu wanakikosoa katika DFB. Ni mzunguko ambao unawahusu wao tu, na kinachoendelea nje sio muhimu," amesema.