1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgombea wa upinzani adai ushindi Tunisia

Mohammed Khelef22 Desemba 2014

Wagombea wote wawili wa urais kwenye uchaguzi wa marudio Tunisia, wamejitangazia ushindi, hali inayozua wasiwasi kwenye taifa hilo la kwanza la Kiarabu kuanzisha vuguvugu la umma dhidi ya watawala.

https://p.dw.com/p/1E8Tb
Wagombea urais wa Tunisia, Moncef Marzouki (kushoto) na Beji Caid Essebsi.
Wagombea urais wa Tunisia, Moncef Marzouki (kushoto) na Beji Caid Essebsi.Picha: F. Belaid/AFP/Getty Images

Ni timu ya kampeni ya mwanasiasa mkongwe Beji Caid Essebsi ndiyo iliyoanza kujitangazia ushindi wa mgombea wao usiku wa jana, ambapo mara tu baada ya vituo vya uchaguzi kufungwa, meneja wa kampeni wa Essesbi, Mohsen Marzouk, alitangaza kuwa Essebsi ameshinda.

"Kwa mujibu wa dalili za awali kutoka kwenye vituo vya kupigia kura, tunaweza kusema kwamba Beji Caid Essebsi anashinda duru ya pili," alisema Marzouk.

Kauli hiyo ilipokewa kwa furaha kubwa na wafuasi wa Essebsi, mmoja wao akisema kwamba hicho ndicho hasa walichokitarajia, lakini nao wafuasi wa rais wa sasa, Moncef Marzouki, walikusanyika kwenye mitaa ya mji mkuu Tunis, usiku huo huo kumuunga mkono kiongozi wao.

Moncef akataa kushindwa

Akizungumza na wafuasi hao waliokuwa wakipiga mayowe na kupeperusha bendera ya Tunisia, Marzouki aliwaambia hakubaliani na tangazo la ushindi la Essebsi.

Wafuasi wa Moncef Marzouki kwenye mkutano wa kampeni.
Wafuasi wa Moncef Marzouki kwenye mkutano wa kampeni.Picha: Getty Images/AFP/B. Taieb

"Tangazo hilo linawakilisha ukosefu wa demokrasia na tunapaswa kungojea ikiwa tunataka kuwa sehemu ya sheria ya nchi. Ninataka kuwaambia kwamba sisi ni washindi, ndio washindi na ni washindi. Tunisia imeshinda na nyinyi ni washindi, nyinyi ni washindi kwa ajili ya Tunisia, kwa ajili ya demokrasia na kwa ajili ya haki," alisema Moncef Marzouki.

Matokeo rasmi yanatazamiwa Jumatatu (22 Disemba).

Endapo ushindi wa Essebsi aliyekuwa spika wa bunge chini ya utawala wa Ben Ali utathibitishwa, utamuwezesha mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 88 kujikusanyia madaraka kikamilifu, kwani chama chake cha Nidaa, kisichofuata siasa za kidini, tayari kinalidhibiti bunge baada ya kukishinda chama cha Ennahda, chenye misingi ya Uislamu, hapo mwezi Oktoba.

Kiwango kidogo cha wapigakura

Hata hivyo, katika awamu ya kwanza ya uchaguzi, asilimia 70 ya wapigakura walijitokeza kupiga kura zao, lakini kwenye uchaguzi wa Jumapili (21 Disemba) wa marejeo, ni asilimia 59, kutokana na kile wapigakura wengi wanachosema ni kupoteza imani na wasiasa.

Wafuasi wa Moncef Marzouki kwenye mkutano wa kampeni.
Wafuasi wa Moncef Marzouki kwenye mkutano wa kampeni.Picha: Getty Images/AFP/B. Taieb

Ikiwa na katiba inayotajwa kuwa ya kimaendeleo na baada ya kupitia kwenye chaguzi kadhaa kwa mafanikio, Tunisia inasifiwa kuwa mfano wa mageuzi ya kidemokrasia kwenye eneo zima la ulimwengu wa Kiarabu, ambalo bado linapigania kutulizanisha hali baada ya Vuguvugu la mwaka 2011.

Takribani kwenye nchi zote zilizokumbwa na wimbi hilo, kumekuwa na kiwango kikubwa cha kurudi nyuma, ikiwemo ukandamizaji wa serikali na hatua ya jeshi la Misri kumuangusha rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, Mohammed Mursi. Nchini Tunisia, mapambano yote yaliendelea kubakia kwenye utaratibu wa kisheria.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba