1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wapamba moto Lebanon-mapigano yazuka mitaani

Saumu Mwasimba9 Mei 2008

Saudi Arabia imeitisha kikao cha dhararu cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu kujadili hali inayoikabili Lebanon.

https://p.dw.com/p/DxCX
Kiongozi wa Hezbollah, Hassan NasrallahPicha: AP

Mwito huo wa Saudi arabia umetolewa huku mapigano kati ya Hezbollah na wafuasi wa serikali yakiingia siku ya tatu katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo Beirut.Watu kumi wameuwawa katika mapigano hayo huku wanamgambo wa kundi la Hezbollah wakiwa wameyateka maeneo ambayo ni ngome ya wasunni wanaoiunga mkono serikali inayoegemea upande wa Marekani.Aidha wanamgambo wa Hezbollah wanaungwa mkono na Iran wamekifunga kituo cha televisheni pamoja na gazeti linalomilikiwa na serikali .

Kundi la washia la Hezbollah pamoja na washirika wake sasa wanadhibiti karibu nusu ya maeneo yote ya mji mkuu Beirut kasoro wilaya moja tu ambako wapiganaji wafuasi wa serikali wamesalimu amri na kuingia katika mazungumzo ya amani na Hezbollah.Duru za usalama mjini Beirut zimedokeza kwamba wapiganaji wa kundi la wasunni la Tarek al Jadeedi ambao wanaegemea upande wa serikali wamefanya mawasiliano na Hezbollah na kuarifu kuwa tayari kuachana na mapigano dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah.

Magazeti nchini humo leo hii yamechapisha ripoti za kuwaonya walebanon kwamba huenda wakatumbukia katika vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe.Gazeti moja la Ufaransa limeandika kwamba serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na nchi za magharibi inakabiliwa na mtihani mgumu kati ya kufuata mkondo wa amani au kuingia kwenye vita katika mvutano mkubwa na kundi la Upinzani likiongozwa na Hezbollah.

Mapigano yameingia siku ya tatu nchini humo na duru za usalama zimefahamisha kwamba kiasi cha watu 10 wameshauwawa.Roketi zimevurumishwa dhidi ya makaazi ya Saad al Hariri anayeongoza kundi lenye wingi mkubwa bungeni na mwanawe waziri mkuu wa zamani aliyeuwawa Rafiq Hariri.hata hivyó hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Mapigano makali ya risasi pia yameripotiwa katika maeneo kama Hamra yanayokaliwa na mchanganyiko wa wasunni ,washia na wakristo ambako pia wanamgambo wa upinzani wanaonekana kuchukua udhibiti.Kufuatia hali hiyo ya mapigano ambayo yanahofiwa huenda yakazidi na kusababisha vita kamili vya kimadhehebu ndani ya Lebanon jumuiya ya kimataifa imetoa mwito wa kudumishwa utulivu .

Saudi Arabia ambayo ni nchi yenye usemi mkubwa katika eneo hilo na ambayo inaiunga mkono serikali ya Fuad Siniora imeitisha mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu kujadiliana hatua zakuchukuliwa katika mzozo huu kabla mambo hayaharibika zaidi.

Marekani kwa upande mwingine imesema Hezbollah inabidi lifanye uamuzi kuwa kundi la kigaidi au chama cha kisiasa na wala sio kufuata njia zote mbili.

Mapigano kati ya Hezbollah na vikosi vya serikali yaliibuka tangu jumatano wakati wa mgomo wa kitaifa juu ya kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa na kima cha chini cha mishahara.

Lakini mapigano hayo yalipata makali zaidi hapo jana jioni kufuatia madai ya kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah kwamba hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya shughuli za kundi hilo ni sawa na kutangaza vita dhidi ya kundi hilo.

Nasrallah alitoa matamshi ya kupinga hatua ya serikali ya kuanzisha uchunguzi dhidi ya vyombo binafsi vya mawasiliano vinavyoendeshwa na Hezbollah.