Mgogoro wa Zimbabwe katika awamu mpya
23 Juni 2008Mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe umeingia awamu nyingine kufuatia kujiondoa kwa kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai katika kinyang'anyiro hicho akisema hali ilivyo kwa sasa haimruhusu kuendelea .
Sasa amekimbilia katika ubalozi wa moja wa nchi za magharibi mjini Harare.
Matukio katika awamu hii yanakuja moja baada ya lingine.Baada ya Tsvangirai kutangaza kuwa amejiondoa na kumuachia mwanya rais Mugabe sasa mengine yamefuata.
Habari mpya zinasema kuwa sasa Tsvangirai amekimbilia katika ubalozi wa Uholanzi mjini Harare.
Msemaji wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Uholanzi amesema kuwa kwa sasa Bw Tsvangirai yuko ubalozini na atakaa huko kwa mda.
Msemaji huyo amesema kuwa ombi lake la kutaka kukaa huko lilitolewa jumapili.
Na jana pia ndio kilikuwa chanzo cha misururu ya matokeo mengi ya leo jumatatu.
Aliuambia mkutano wa wandishi habari kuwa amejindoa katika kinyang'anyiro hicho.Miongoni mwa sababu alizotoa ni kuwanyanyansa wafuasi wake.
Kuna taarifa zinazosema kuwa serikali imemtaka abadili uamuzi wake huo,lakini inasekema hajakubali.George Chiramba ni msemaji wa rais Mugabe.Asema ikiwa hatua ya Tsvangirai ya kujiondoa inamsumbua rais Mugabe.Amesema kuwa hilo halimsumbui Mugabe kwani yeye anaendelea na kampeini zake,yeye anavyoelewa ni kuwa uchaguzi unaendelea kama ilivyopangwa.
Tsvangirai kwa upande wake ameiambia redio moja ya Marekani kuwa angetaka jumuia ya kikanda ya SADC,ifanye kila juhudi kuona kama uchaguzi unaahirishwa na kufanyika chini ya viwangovya jumuia hiyo.Vinginevyo,amesema kuwa jumuia hiyo imshinikize Mugabe akubali kushindwa katika duru ya kwanza na kuwa achie madaraka.
Na leo jumatatu asubihi polisi wa kuzuia fujo wamevamia makao makuu ya chama chake na kuwachukua watu kadhaa ambao ni wahanga wa ghasia za sasa za nchini humo ambao walikuwa wametafuta hifadhi katika makao hayo yanayopatikana katika jengo la Harvest House katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Harare.
Afisa mmoja wa chama cha MDC,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa chama chake hakijaelewa ni kwa sababu gani ofisi zao zimevamiwa na pia ni kwa nini watu hao wamekamatwa.
Upinzani unasema kuwa zaidi ya wafuasi wake 80 wameuawa huku maelfu kadhaa kujeruhiwa katika ghasia za kisiasa.Baadhi ya wahanga inaaminika kutafuta hifadhi katika makao makuu ya MDC.Lakini polisi imeyavamia na kuwachukua baadhi yao.Taarifa zinasema waliochukuliwa na polisi katika uvamizi wa jumatatu wanafikia 60.