Mgogoro wa Yemen wazidi kuzusha wasiwasi Kimataifa
21 Januari 2015►Hata hivyo duru hazijaeleza hadi wakati huu nini kilichozungumzwa kati ya rais Hadi na mwakilishi húyo.Pamoja na hayo kuna taarifa za kufungwa uwanja wa ndege mjini Aden kusini mwa Yemen pamoja na kutekwa nyara kambi ya kijeshi inayotumiwa kuhifadhi makombora ya masafa marefu.
Taarifa zimesema rais Mansur Hadi amempokea Saleh al-Samad katika makaazi yake huko magharibi mwa mji mkuu Sanaa huku ikitajwa pia rais huyo alikutana na washauri wengine pamoja na machifu wa kikabila,ingawa kilichozungumzwa hakikutajwa.
Sammad alikuwa ni mshauri wa rais Hadi chini ya makubaliano yaliyotiwa saini septemba 21 wakati wahouthi walipotwaa mamlaka ya mji mkuu Sanaa. Hata hivyo kuna mkutano mwingine mkubwa zaidi utakaowajumuisha wawakilishi wa pande zote za kisiasa utakaofanyika baadae leo(21.01.2015) mbele ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa Jamal Benomar.
Mazungumzo hayo yanakuja katika wakati ambapo Jumanne yalishuhudiwa mapigano makali kati ya wanamgambo hao wahouthi na wanajeshi wanaolinda makaazi ya rais wakati huohuo ikitajwa kwamba wapiganaji hao waliiteka ikulu ya rais. Leo Jumatano pia washauri wawili wa rais Hadi wametoa taarifa zinazosema kwamba waasi hao wakishia wanaoendeleza mapambano ya kuwania madaraka wanamshikilia mateka rais Hadi nyumbani baada ya hapo jana kuidhibiti Ikulu.
Jumuiya ya Kimataifa imeingiwa na wasiwasi juu ya ulipofikia mgogoro huu,baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura jana jioni kulaani ghasia zinazotokea na kutoa mwito wa kufikiwa amani ya kudumu.Marekani imesema inaendelea kumuunga mkono rais Hadi na serikali yake na kutoa mwito wa kusitishwa vita mara moja.Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Mark Lyall Grant pia ametoa mwito kama huo.
Wanachama wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba limewataka waasi wa Houthi kuondoka mjini Sanaa.Wakati huohuo rais aliyeondolewa kwa nguvu madarakani nchini humo Ali Abdalla Saleh ambaye anatajwa kuwa nyuma ya waasi hao wa Houthi amemshauri rais Hadi kupitia taarifa fupi kuitisha uchaguzi wa mapema ili kuepusha balaa kubwa zaidi.Kiongozi wa waasi Abdel-Malek al-Houthi aliyehutubia taifa jana usiku alisema kinachotokea ni hatua ya mapinduzi inayolenga kumlazimisha rais Hadi atekeleze makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambayo yanatoa madaraka makubwa zaidi kwa wahouthi.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Iddi Ssessanga