Mgogoro wa Yemen wazidi kutisha
24 Machi 2015.Tayari Saudi Arabia imesema hatua mwafaka zitachukuliwa kuIlinda kanda hiyo dhidi ya kile ilichokiita mabavu ya washirika wa Iran yaani wahouthi.
Hatua iliyoitishwa na waziri wa mambo ya nje wa Yemen Riyadh Yaseen inaweeza ikazitumbukiza nchi jirani katika mgogoro wa kuwania madaraka ambao unazidi kutanuka.Waziri huyo wa mambo ya nje akizungumza jana na gazeti la al-Sharq al Awsat alitowa mwito wa nchi sita za baraza la ushirikiano wa eneo la ghuba kuingilia kati kijeshi mgogoro huu ili kuwashinda wahouthi.
Halikadhalika alitowa kauli kwamba ameshautayarifu Umoja wa Mataifa pamoja na Jumuiya ya Kimataifa juu ya ulazima wa kutengwa eneo lisilokubaliwa ndege kuruka pamoja na kuzuiwa matumizi ya ndege za kijeshi kwenye viwanja vya ndege vinavyodhibitiwa na wanamgambo wakihouthi.
Wahouthi ambao wanafikra sawa na Iran waliudhibiti mji mkuu Sanaa tangu mwezi Septemba hiyo ikiwa ni hatua ya kipigo kikubwa kwa serikali ambayo inashuhudia mpasuko mkubwa ndani ya jeshi.Kundi hili awali lilikuwa likigawana madaraka na rais Manour hadi lakini akalivunja bunge mwezi uliopita.
Saudi Arabia na nchi nyingine jirani za kiarabu zinaitazama hatua hiyo ya kutwaa madaraka kama mapinduzi na zinaamini Iran inajaribu kujenga himaya yake katika kanda hiyo kwa kuyaunga mkono makundi yenye silaha yanayoegemea upande wake.Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Saud al-Faisal ameonya akiwa mjini Riyadh kwamba Iran inajaribu kujenga chuki za kimadhebeu katika kanda hiyo na kusema nchi za Ghuba za Kiarabu zitachukuwa hatua kumuunga mkono rais Hadi.
Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Phillip Hammond aliyekuwa pamoja katika mkutano na waandishi wa habari na mwenzake al Saud alirudia mwito wa kuyataka makundi yote yanayopingana ikiwemo wahouthi kushiriki mazungumzo ya amani nchini Saudi Arabia.Lakini pia akasisitiza kusema na hapa tunanukuu
''Msimamo wa Uingereza uko wazi kabisa katika kumuunga mkono rais hadi,serikali halali ya Yemen na uhalali wa dola la Yemen.Lakini hili sio suala tunaloweza kuliamulia peke yetu.Tutashirikiana na Saudi Arabia na washirika wake wa nchi za baraza la ushirikiana la ghuba,Marekani,Ufaransa na nyingine zinahusika,kupitia kile kinachoitwa marafiki wa Yemen ambacho sisi ni mwenyekiti mwenza.''
Hammond alisema Uingereza na washirika wake wanajadiliana kuhusu hatua ya kuchukua.Yote haya yamejitokeza katika wakati ambapo bado mapigano yamekua yakiendelea kushuhudiwa,wanamgambowakihouthi walipambana na makundi hasimu upande wa kusini na katikati ya Yemen jana Jumatatu.
Walioshuhudia wameripoti kwamba wapiganaji wakihouthi wakiungwa mkono na vitengo kadhaa vya wanajeshi walifyetuliana risasi katika mapambano na wapiganaji kutoka makabila ya mkoa wa Taiz ambayo yanamuunga mkono rais Hadi.
Mapigano pia yalizuka kati ya wahouthi na wanamgambo wa kikabila kwenye mikoya ya Al-Bayda na Mareb ambako kiasi watu 15 kutoka pande zote waliuwawa.Siku ya Jumapili wahouthi waliuteka mji wa Taiz abao ni mji wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen hatua iliyowashtuwa wapinzani wa kundi hilo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/rtre/ape
Mhariri:Mohammed AbdulRahman