1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Mali waendelea

10 Agosti 2012

Serikali ya Mali imeeleza kwamba hivi sasa matumizi ya nguvu ya kijeshi katika eneo la Kaskazini, linaloshikiliwa na wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali, haiepukiki.

https://p.dw.com/p/15nka
Waasi wa kundi la mujao
Waasi wa kundi la mujaoPicha: Getty Images

Kundi linalojiita vuguvugu la kutaka umoja na vita vya Jihad katika Afrika Magharibi, kwa kifupi Mujao, lilimkata mkono mwizi mmoja na kusema kwamba limefanya hivyo kwa kufuata sheria za Kiislamu. Watu walioshuhudia tukio la mwizi kukatwa mkono, walieleza kwamba damu nyingi sana ilimwagika baada ya mwizi huyo aliyeiba pikipiki kukatwa mkono na wafuasi wa kundi la Mujoa kwenye mji wa Ansongo. Kundi hilo linataka kupitisha matumizi ya sheria ya kiislamu kuwa sheria inayotumika katika nchi nzima ya Mali. Kuanzia mwezi wa Aprili waasi wa Mujao pamoja na makundi mengine ya waislamu wenye itikadi kali, wamekuwa wakilitawala eneo la Kaskazini la Mali. Kwa sababu hiyo, nchi jirani sasa zinauwekea shinikizo utawala wa nchi hiyo, ili uharakishe kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea.

Waziri wa maendeleo na misaada ya kigeni wa Ujerumani, Dirk Niebel, ameeleza kwamba hali ya kibinadamu iliyopo nchini Mali haikubaliki. Niebel aliyasema hayo alipokuwa katika mji mkuu wa Mali, Bamako, hapo jana. Hata hivyo, waziri huyo alikiri kwamba serikali ya nchi yake kwa sasa haiwezi kutoa msaada kwa watu waishio kaskazini mwa Mali. "Hivi sasa tunatoa misaada isiyopitia serikalini bali inayowafikia raia moja kwa moja," alisema Niebel." Kwa sasa hatuwezi kutoa misaada hiyo kwa sababu ya hali ya usalama. Tutaendelea kutoa ushirikiano wa kimaendeleo utawala wa kikatiba utakaporejeshwa."

Mali yashindwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa

Lakini hili litawezekanaje? Hadi sasa, Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mali. Hata hivyo, Jumuiya hiyo inafanya majadiliano katika maeneo matatu: Kwa upande mmoja imeitaka serikali ya mpito iunde serikali ya umoja wa kitaifa. Pili, ECOWAS inajadili na waislamu wenye itikadi kali wanaolitawala eneo la Kaskazini na wenye lengo la kulibadili taifa zima la Mali kuwa taifa linalotawaliwa na sharia. Kwa upande wa tatu, jumuiya hiyo inatishia kutumia nguvu za kijeshi kulikomboa eneo la Kaskazini mwa Mali.

Dirk Niebel akiwa na Cheikh Modibo Diarra
Dirk Niebel akiwa na Cheikh Modibo DiarraPicha: picture-alliance/dpa

ECOWAS iliipa serikali ya Mali muda hadi leo hii kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, jambo ambalo halijafanyika. Dirk Niebel anatumaini kwamba hatua hiyo itachukuliwa katika siku 10 hadi 14 zijazo.

Katika eneo la Kaskazini la Mali, hali ya kibinadamu inazidi kudorora. Kati ya raia 280,000 na 300,000 wameyakimbia makaazi yao. Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yameonya kwamba misaada ya haraka inahitajika. Ujerumani imefuata wito huo na kuahidi kuwapelekea wakaazi wa eneo hilo msaada wa chakula.

Mwandishi: Peter Hille/Elizabeth Shoo

Mhariri: Yusuf Saumu