1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kisiasa Lebanon wafikia pabaya

Mohamed Dahman13 Machi 2008

Haijulikani kwa kiasi gani Marekani itajiingiza Lebanon kukwamuwa mchakato wa kisiasa ulioilemaza nchi hiyo na kila mtu ana hofu kwamba vita vinakuja.

https://p.dw.com/p/DNiJ
Nafiasi ilioachwa na Rais Emile Lahoud bado iko waziPicha: AP

Mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon watazamiwa kupamba moto wakati nchi hiyo iliokwama kuendesha shughuli zake rasmi za kiserikali ikiwa imegawika kati ya serikali ya Siniora inayoungwa mkono na Marekani na vyama vya upinzanivinayoongozwa na kundi la Hezbollah na Generali wa KikristoMichel Aoun ambao wanaungwa mkono na Syria na Iran.

Kura ya bunge kwa ajili ya mtu wa kushika wadhifa wa urais anayeafikiwa na pande zote ambaye ni mkuu wa majeshi Michel Suleiman imecheleweshwa kwa mara ya 16 wiki hii na kuifanya nafasi hiyo kuwa wazi tokea Rais Emile Lahoud aliekuwa akiungwa mkono na Syria kumaliza muda wake hapo mwezi wa Novemba mwaka jana.

Serikali ya Waziri Mkuu Fouad Siniora inashinikiza kupigwa haraka kwa kura hiyo ya urais na ufafanuzi wa kugawanya madaraka ushughulikiwe baadae wakati upinzani ukidai kufikiwa kwanza kwa ufumbuzi wa masuala muhimu.

Uchumi wa Lebanon umeshuka na uwezekano wa vita kwa wananchi wenye hofu umeongezeka baada ya kuuwawa kwa Kamanda wa Hezbollah Imad Mughniyeh na dalili za Hezbollah kuwa tayari kwa vita vya wazi na Israel mtuhumiwa mkuu wa mauaji ya kamanda wao huyo.

Mughniyeh anaelezwa kuwa alikuwa kamanda mwandamizi wakati wa vita na Israel hapo mwaka 2006 na kuuwawa kwake hapo tarehe 26 Februari katikati ya mji mkuu wa Syria Damascus kumetowa pigo kubwa kwa wasi wasi wa usalama wa Hezbollah na Syria.

Kuwekwa kwa meli ya kivita ya Marekani USS Cole nje ya fukwe za Lebanon hapo tarehe 28 Februari kulinda utulivu wa kisiasa kumezusha hofu miongoni mwa Walebanon.

Alistair Crooke mshauri wa zamani wa Mashariki ya Kati wa mwakilishi wa Umoja wa Ulaya Havier Solana anasema kuwasili kwa meli hiyo kuunga mkono serikali tawala ya mseto ya Siniora kumekuwa na taathira ya mparaganyiko wa mawazo kwa watu.

Crooke anakumbusha kwamba mara ya mwisho meli ya kivita ya Marekani kuingia kwenye bahari ya Lebabnon ilikuwa ni wakati wa vita vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe hapo mwaka 1983 kwa niaba ya rais wa wakati huo Amin Gemayel.

Meli hiyo iliipiga mabomu Beirut na milima ya Chouf kutoka ufukweni.

Meli ya USS Cole tayari imeondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na manowari sita za kundi la washambuliaji la wanamaji wa Marekani zikiongozwa na meli ya kivita USS Nassau.

Kwa upande wake Ahmad Moussalli profesa wa mafunzo ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Marekani mjini Beirut ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kwamba anadhani ujumbe wa meli ya USS Cole ulikuwa ni kwa eneo la Mashariki ya Kati na sio wa ndani mwa Lebanon kwamba ni ujumbe wa ishara kwa Hezbollah na wale wanaoiunga mkono kutojibu mapigo kwa ulipizaji kisasi mkubwa sana kutokana na mauaji ya kamanda Mughniyeh.

Anasema kwa hakika Hezbollaha haitaki vita vyengine lakini kutokana na hicho kilichotokea kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameahidi kuchukuwa hatua fulani na anajulikana kwa kutenda kile anachosema.

Timur Goksel msemaji wa zamani wa muda mrefu na mpatanishi akiwa na kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa huko kusini mwa Lebanon UNIFIL anaamini kwamba vita vengine kati ya Israel na Hezbollah vitakuwa tafauti, vitakuwa na umwagaji damu zaidi na uharibifu mkubwa.

Kutokana na Umoja wa Waarabu kushindwa kuutatuwa mgogoro wa kisiasa wa Lebanon na kurefusha kutokuwepo kwa rais au serikali ya umoja wa kitaifa vyama vya kisiasa nchini humo vinaendelea kutafautiana sana juu ya namna ya kusonga mbele.

Upinzani unadai kurekebishwa kwa uwiano wa viti bungeni wakitaka kupatiwa theluthi mojya ya viti hivyo na uwezo wa kupiga kura ya turufu kadhalika marekebisho juu ya nyadhifa za wizara.

Mataifa ya magharibi yanataka tu rais achaguliwe wakati upinzani unapinga kwamba jambo hilo itakuwa ni kutibu dalili za tatizo ni sio sababu ya tatizo.