Mgogoro wa kisiasa Catalonia unazidi kupanuka
24 Oktoba 2017Rais wa Catalonia Carles Puigdemont ameliomba bunge kujadili na kupiga kura ya namna ya kuujibu mpango wa serikali kuu ya Uhispania, uliyotangazwa siku ya Jumamosi na Waziri Mkuu Mariano Rajoy. Bunge hilo limepanga kuandaa mjadala huo siku ya Alhamisi. Aidha Rajoy anataka kutumia kipengee cha 155 katika katiba ya nchi hiyo kinachoridhia serikali kuu kuingilia kati na kuiendesha Catalonia, baada ya serikali ya jimbo hilo kudai mamlaka ya kujitenga na Uhispania, kufuatia kura ya maoni ya Oktoba mosi iliyokuwa imepigwa marufuku.
Hotuba ya siku ya Jumamosi ya Rais Puigdemont imeonekana na wengi kama kitisho cha kutangaza uhuru wao. Hata hivyo serikali ya Uhispania imesema hakuna mazungumzo yanayowezekana iwapo suala la uhuru wa Catalonia bado lipo mezani, huku ikiwa na nia ya kuwafuta kazi maafisa wote wa Catalonia na kuitisha uchaguzi wa mapema katika jimbo hilo.
Mjini Madrid kwenyewe, vyama vya kisiasa vimewateua maseneta 27 kuangalia mchakato wa ombi la serikali la kutaka kutumia kipengee hicho nambari 155 cha katiba. Kundi hilo linawajumuisha wanachama 15 kutoka upande wa chama tawala cha Popular Party, hii ikimaanisha suala hilo bila shaka litaidhinishwa.
Kulingana na Naibu Waziri Mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de Santamaria, pindi bunge la senate litakapopitisha mpango huo, mamlaka ya serikali ya Catalonia itamalizika papo hapo, Rais hatolipwa tena mshahara wake na hatakuwa na mamlaka ya kuamua chochote. De Santamaria amesema serikali kuu inaweza pia kuchukua hatua nyengine iwapo viongozi wa Catalonia wataamua kupuzilia mbali uamuzi utakaopitishwa.
Kwa upande mwengine Wacatalonia wanaotaka kujitenga wamepanga kufanya maandamano makubwa dhidi ya uamuzi wa serikali ya Uhispania iwapo itaendelea na mpango wake wa kutaka rais wao kuachana na mpango wa kutaka uhuru wa eneo hilo. Wazima moto, walimu na wanafunzi wameuingilia mgogoro huo wakionya kufanyika migomo na maandamano wakati Uhispania ikikabiliana na mgogoro wa miongo mingi wa kisiasa unaoikumba nchi hiyo.
Serikali ya Catalonia imesema ina imani maafisa wote wakiwemo polisi hawatakubaliana na mpango wa Uhispania wa kuweka utawala wa moja kwa moja katika jimbo lake jambo linalohofiwa kuleta mgongano miongoni mwa washirika wa Uhispania barani Ulaya.
Wakati huohuo Halmashauri ya Ulaya imesema leo haijabadilisha msimamo wake juu ya Catalonia baada ya matamshi ya Mariano Rajoy ya kutumia madaraka maalum ya katiba kuifuta serikali ya jimbo hilo na kushinikisha uchaguzi mpya ndani ya miezi sita. Msemaji wa kamisheni hiyo amesema msimamo wao unajulikana na wamekuwa wakisema kila kukicha kwamba wanaheshimu katiba na mipango inayofuata sheria ya Uhispania.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/dpa/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman