Mgogoro wa kandanda la Uhispania watokota
9 Mei 2015Hatua hiyo inatokana na mgogoro na serikali kuhusiana na sheria mpya ya haki za matangazo ya televisheni. Rais wa Ligi ya Uhispania Javier Tebas ambaye uhusiano wake na rais wa RFEF Angel Maria Villar umevunjika, amewasilisha mahakamani jana kesi ya kupinga kile amektaja kuwa ni mgomo usio halali.
Awali, serikali ya Uhispania ilionya kuwa kitisho cha wachezaji kandanda nchini humo kufanya mgomo kuhusiana na mgogoro wa kugawana utajiri wa haki za kuonyesha mechi moja kwa moja kwenye televisheni kinaathiri mchezo huo pamoja na mapato yake makubwa.
Wachezaji kutoka timu kubwa nchini humo, zikiwemo Barcelona na Real Madrid, wameungana na kitisho cha kususia michezo ya mwisho ya msimu ikiwa serikali haitafanya upya mashauriano ya mageuzi ya haki za matangazo ya kandanda ya televisheni.
Waziri mdogo wa michezo wa Uhispania Miguel Cardenal amesema ulimwengu wa kandanda una wasiwasi kuhusiana na fursa zitakazopotea na uharibifu ambao kitisho hicho cha mgomo tayari kinaifanyia taswira ya kandanda na uwezo wake wa kujiuza kimataifa.
Shirikisho la RFEF ambalo linasimamia kandanda ya Uhispania na chama cha wachezaji – AFE limetishia kufanya mgomo kuanzia Mei 16. Wanasema hawafurahishwi na jinsi sheria mpya inavyogawa upya mapato kwa kuuza haki za matangazo ya televisheni kwa michezo ya faida kubwa ya ligi kuu ya kandanda nchini Uhispania.
Serikali inasisitiza kuwa mageuzi hayo yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanatoa fursa nzuri kwa vilabu maskini vya daraja ya chini, lakini shirikisho la kandanda na wachezaji wanasema hiyo haitoshi. Mpango huo unazipa nafasi kampuni za utangazaji kutoa maombi ya pamoja ya haki za kurusha matangazo ya michuano badala ya kuviacha vilabu kushauriana na kila chombo cha habari kama ilivyokuwa hapo awali. Mfumo huo wa awali ulivinufaisha vilabu tajiri na vyenye mafanikio makubwa zaidi Real na Barcelona.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu