1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Ivory Coast wajadiliwa mjini Abuja

Abdu Said Mtullya23 Machi 2011

Viongozi wa Ecowas wakutana kuujadili mgogoro wa Ivory Coast

https://p.dw.com/p/10gSP
Laurent Gbagbo anaeendelea kuyang'ang'ania madaraka nchini Ivory CoastPicha: picture alliance/landov

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wanakutana katika mji Mkuu wa Nigeria ,Abuja,katika juhudi za kuutatua mgogoro wa Ivory Caost

Kikao hicho cha siku mbili kinafanyika wakati ambapo pana tishio kubwa la kuzuka vita vya wenyewe kwa nchini humo.

Viongozi hao wa jumuiya ya uchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika, Ecowas, wanakutana miezi mitatu baada kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo, ambae bado anayang'ang'ania madaraka, licha ya kushindwa katika uchaguzi na mpinzani wake, Allasane Ouattara, anaetambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa mshindi wa uchaguzi.

Viongozi wa jumuiya ya Ecowas wamebanwa na wanatakiwa wachukue hatua za kuutatua mgogoro wa Ivory Coast.

Akikifungua kikao hicho mjini Abuja, Rais Jonathan Goodluck wa Nigeria, ambae ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya Ecowas, amesema jumuiya hiyo inafikiria kuuomba Umoja wa Mataifa uchukue hatua ndefu zaidi juu ya Ivory Coast.Rais Goodluck amesema viongozi wa Ecowas wanaweza kupitisha azimio juu ya kuutaka Umoja wa Mataifa upanie zaidi, na ameeleza matumaini juu ya kufikiwa suluhisho bila ya matumizi ya nguvu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mjini Abuja, wanawake wapatao mia moja walifanya maandamano nje ya makao makuu ya jumuiya ya Ecowas katika mji huo ya kuwataka viongozi wao wachukue hatua za kukomesha umwagikaji damu nchini Ivory Coast.

Jumuiya hiyo ya Ecowas pia inamtambua kiongozi wa upinzani Allassane Outtara kuwa Rais wa Ivory CoastLakini Rais wa hapo awali, Laurent Gbagbo, anakataa kuondoka madarakani wakati ambapo nchi yake imezidi kudidimia katika mgogoro.

Meja wa wanajeshi wanaomuunga mkono Outtara ,Daounda Doumbia, amesema nguvu zinaweza kutumiwa ikiwa Gbagbo hatajing'atua.Msemaji wa jumuiya ya uchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika, Ecowas, amejaribu kuiweka katika kiwango cha chini, hatari ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast na amesema tu kwamba Umoja wa nchi za Afrika unaimarisha juhudi za kuleta suluhisho nchini humo.

Msemaji huyo, Sunny Ugoh, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jumuiya ya Ecowas itaendeleza juhudi za nchi za Umoja wa Afrika.

Hapo awali, waziri wa mambo ya nje wa Nigeria, Odein Ajumogobia aliutaka Umoja wa Mataifa uidhinishe matumizi ya nguvu ili kumwondoa Gbagbo madarakani.

Mwandishi:Mtullya, Abdu/AFPE/ZAR

Mhariri: Miraji Othman