1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Euro waleta serikali mpya Ulaya lakini siasa zile zile

29 Novemba 2011

Hadi hivi sasa, mzozo wa fedha ulioibuka mwaka 2007 kote duniani, umeshasababisha serikali mpya kuchaguliwa katika baadhi ya nchi za Ulaya - lakini ionekanavyo, sababu halisi za mzozo huo wa fedha bado hazikuondoshwa.

https://p.dw.com/p/13Iwe
Mgogoro wa sarafu ya euro waweza kuleta serikai mpya barani Ulaya, bali sio siasa tafauti
Mgogoro wa sarafu ya euro waweza kuleta serikai mpya barani Ulaya, bali sio siasa tafautiPicha: picture-alliance/dpa/DW

Uhispania iliyokuwa na uchaguzi Novemba 20, ni nchi ya tano katika Umoja wa Ulaya na kanda ya euro, kufululiza kupata serikali mpya. Hayo ni matokeo ya mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na kusambaratika kwa masoko ya fedha kote duniani katika mwaka 2007. Hata Iceland na Hungary ambazo hazimo katika kanda ya euro, zimepata serikali mpya tangu mwaka 2007 - hayo yakiwa ni matokeo ya mzozo wa fedha na madeni ya serikali.

Kwani, ionekanavyo, raia waliopiga kura wala hawakuzingatia sera za vyama, bali walivipigia kura vyama vya upande wa upinzani bila ya kujali iwapo ni vya mrengo wa kulia au shoto - walichokitaka ni kimoja tu: kuzitimua serikali zilizokuwa madarakani bila ya kuzingatia miradi au ufanisi wa serikali hizo. Serikali mpya zimeshika madaraka nchini Iceland, Ireland, Ureno, Hungary na Uhispania baada ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia.

Wakati huo huo, nchini Ugiriki na Italia, serikali za George Papandreou na Silvio Berlusconi zililazimishwa kujiuzulu kwa sababu ya kutofanikiwa kusuluhisha mizozo ya madeni. Nafasi zao zimechukuliwa na serikali zilizoundwa hasa na wataalamu wa kiuchumi, bila ya kupigiwa kura na umma. Lakini mabadailiko hayo yote hadi sasa hayakuleta matokeo ya maana katika kupambana na kiini cha mzozo huo wa madeni. Kwa mfano masoko ya fedha ya kimataifa yalio na ushawishi mkubwa na mtindo wa serikali wa kuchukua mikopo kulipia shughuli zake badala ya kuwa na mfumo wa haki wa kutoza kodi ya pato na mali.

Hadi hivi sasa, serikali zote mpya zinapunguza matumizi katika sekta za umma na zimepandisha kodi ya mauzo. Vile vile huenda zikazingatia kuendelea na miradi ya kubana matumizi iliyoanzishwa na serikali za zamani bila ya kujali kuwa hatua hizo huenda zikasababisha uchumi kudorora na hivyo kupunguza uwezo wa serikali kujipatia fedha zaidi. Serikali zote mpya katika kanda ya euro ambazo zimeathirika vibaya kiuchumi, zinaazimia kuendelea kutumia sarafu ya euro. Hiyo, licha ya tofauti za ushindani wa kiuchumi katika kanda ya euro, kuashiria kuwa mfumo wa sarafu wa hivi sasa hauwezi kuendelea kama ulivyo.

Serkali mpya zinakuja Ulaya lakini haziji na siasa mpya kuelekea mgogoro wa sarafu ya euro.
Serkali mpya zinakuja Ulaya lakini haziji na siasa mpya kuelekea mgogoro wa sarafu ya euro.Picha: Fotolia

Tatizo ni kwamba katika kanda ya euro hakuna mshikamano katika mifumo ya kodi ya nchi tofauti na pia hakuna sera moja ya uchumi. Isitoshe, baadhi ya serikali za nchi za Ulaya zinasita kuchukua hatua za kuyadhibiti masoko ya fedha ya kimataifa, kupiga marufuku biashara kadhaa za fedha zinazozingatia maslahi ya upande mmoja tu na kurejesha mamlaka ya taasisi za kidemokrasia za umma badala ya maslahi ya binafsi.

Mwandishi: Prema Martin/IPS
Mhariri: Josephat Charo