1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro baina ya Uturuki na Marekani watokota

14 Agosti 2018

Wiki iliyopita Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kodi mpya zitakazotozwa vyuma na alumini kutoka Uturuki, kufuatia hasira yake iliyotokana na hatua ya kuendelea kuzuiliwa kwa Kasisi Andrew Brunson jijini Ankara.

https://p.dw.com/p/339nu
USA Präsident Donald Trump in der Militärbasis Fort Drum
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/C. Kaster

Hatua hiyo ya Trump ya kuongeza kodi inayotozwa bidhaa hizo imechangia kudorora zaidi kwa thamani ya Uturuki. Mshauri wa kitaifa wa masuala ya usalama wa Rais Trump, John Bolton alikutana na Balozi Serdar Kilic wa Uturuki siku ya Jumatatu na kujadili hatua ya Uturuki kuendelea kumzuilia mchungaji Andrew Brunson na uhusiano baina ya taifa hilo na Marekani.

Itakumbukwa Ijumaa wiki iliyopita Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Edorgan aliandika katika gazeti la The New York Times na kusema na hapa tunanukuu,"Hadi pale Marekani itakapobadili mwenendo wa kulilenga taifa moja na ukosefu wa heshima, Uturuki itaanza kutafuta wandani na washirika wapya." mwisho wa kumnukuu.

Erdogan amewatolea wito Waturuki watulie wakati nchi ikikabiliwa na mtihani. "Nawashauri wananchi wangu, hasa walio katika biashara. Hatua mwafaka ya kuthibiti athari za kiuchumi ni kuendelea kuchapa kazi. Tutazalisha zaidi na kusafirisha bidhaa zetu zaidi. Kuyafunga maghala yetu na kusitisha uzalishaji hakuna maana na kutakuwa na athari mbaya zaidi, na tutasusia vifaa vya kielektroniki kutoka Marekani."

Türkei Ankara Rede Erdogan
Recep Tayyip Erdogan ambaye ni Rais wa UturukiPicha: picture-alliance/Xinhua/Turkish Presidential Palace

Onyo hilo lilijiri baada ya Erdogan kuzungumza kwa njia ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kujadili uhusiano wa kiuchumi na biashara, vile vile mzozo nchini Syria. Ushirikiano wa kijeshi kati ya Uturuki na Marekani umeathirika kutokana na hatua ya Marekani kuwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria wanaojulikana kama YPG, ambao Uturuki wanalichukulia kuwa kundi lililochipuka kutoka kwa lile wanalolitaja kuwa kundi la kigaidi la PKK.

Mwegemeo wa Uturuki katika NATO watiliwa shaka

Uhusiano wa mataifa ya Urusi na Uturuki umeibua maswali ya iwapo mwegemeo wake katika jumuiya ya kujihami ya NATO unaweza kuaminika, na iwapo iruhusiwe kuendelea kuwa katika muungano huo. Hata hivyo Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Mashariki ya Kati Joshua Landhis ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba "kuondolewa kwa Uturuki katika NATO huenda kukawa na athari kubwa kinyume na inavyodhaniwa. Na iwapo hilo litafanyika, basi itakuwa kuipeleka Uturuki katika mikono ya Urusi."

Wasiwasi ulioongezeka zaidi baada ya Uturuki, licha ya kuwa mshirika wa NATO, kuingia katika makubaliano ya kununua mfumo wa ulinzi wa Urusi wa S-400. Hatua ya aina hiyo itakiuka vikwazo ilivyowekewa Urusi, na uhusiano wa Uturuki na Putin umeishangaza sana Marekani na Umoja wa Ulaya. Jumatatu wiki hii Rais Trump alitia saini sheria ya kuidhinisha ulinzi ambayo inazuia kuwasilishwa kwa ndege ya kivita aina ya F-35 kwa Uturuki, iwapo taifa hilo litaendelea na ununuzi wa mfumo wa ulinzi wa S-400 kutoka Urusi.

Kamanda mstaafu wa jumuiya ya NATO kutoka Marekani, James Stavridis, amezihimiza Uturuki na Marekani zifanye kila linalowezekana kusuluhisha tofauti zao na kuboresha mahusiano. Amesema kuipoteza Uturuki katika NATO litakuwa kosa kubwa lisilo mithili ikizingatiwa muhimu wa Uturuki kisiasa na kijiografia ulimwenguni.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFP

Mhariri: Josephat Charo