1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Asili na mazingiraKorea Kusini

Mgawanyiko mkubwa wajitokeza, mkutano wa kudhibiti plastiki

26 Novemba 2024

Tofauti kali zimeukumba mkutano ulioanza jana Jumatatu kule Busan nchini Korea Kusini, wa kujadili mkataba wa kukabili uchafuzi wa plastiki. Baadhi ya nchi zinahisi rasimu haijazingatia matakwa yao.

https://p.dw.com/p/4nQuh
Japo karibu kila mtu anakubali kuwa uchafuzi wa plastiki ni tatizo, maelewano kuhusu jinsi ya kulitatua, yamesalia kuwa machache.
Japo karibu kila mtu anakubali kuwa uchafuzi wa plastiki ni tatizo, maelewano kuhusu jinsi ya kulitatua, yamesalia kuwa machache.Picha: FRED DUFOUR/AFP

Miongoni mwa masuala yenye utata, ni iwapo mkataba huo utazuia uzalishaji wa plastiki, uwezekano wa kupiga marufuku kemikali zinazohofiwa kuwa sumu kwa afya ya binadamu na jinsi ya kulipia utekelezaji.

Baadhi ya nchi, ikiwemo kile kinachoitwa ‘Muungano wa Matarajio ya Juu' (HAC), ambao unashirikisha mataifa mengi ya Afrika, Asia na Ulaya, zinataka mkataba huo kushughulikia "plastiki kwa upana wake.

Hiyo ikimaanisha kupunguza uzalishaji, kubuni upya bidhaa mbadala zinazoweza kutumika tena na kuchakatwa tena, na kushughulikia taka.

Abdelrahman Al Gwaiz wa Saudi Arabia, aliyezungumza kwa niaba ya kundi la nchi za Kiarabu alionya na kusema "Ukweli ni kwamba nchi nyingi hazijioni kuwa zimewakilishwa katika rasimu hii."

Juhudi za kudhibiti uchafuzi wa plastiki Dar es Salaam

Ukinzano wa muda mrefu kwenye rasimu

Tofauti hizo kubwa zimekumba duru nne za awali za mazungumzo hayo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na hivyo kusababisha ukinzano wa muda mrefu kwenye rasimu ya mkataba huo.

Akifungua mkutano huo, mwanadiplomasia wa Ecuador Luis Vayas Valdivieso, anayeongoza mazungumzo hayo aliyaonya mataifa na kusema

"Mkutano huu ni zaidi ya kuandaa tu mkataba wa kimataifa. Ni kuhusu wanadamu kuwa mbioni kukabiliana na changamoto iliyopo.”

Valdivieso aliwasilisha pendekezo mbadala linalonuia kusawazisha maoni ya wajumbe ili kuendeleza mazungumzo. Lakini nchi kadhaa, ikiwemo Urusi na India, walipinga  pendekezo hilo, mara moja.

Unaweza kusoma pia: Somalia yapiga marufuku mifuko ya plastiki

Akizungumza katika kikao cha wazi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alihimiza upatikanaji wa kile alichokiita "makubaliano ambayo yanashughulikia mzunguko wa maisha yote ya plastiki, hatua za kuondoa plastiki na kukuza nyenzo mbadala.”

Guterres alisema mkataba kama huo utatoa suluhisho madhubuti kwa nchi zote kupata teknolojia na kuboresha mazingira ya ardhini na baharini. Aidha haimwachi mtu yeyote nyuma wakiwamo baadhi ya watu walio hatarini zaidi, kama vile wazoaji na waokotaji taka.

Unaweza kusoma pia: UN yawasilisha mpango wa kupunguza taka za plastiki kwa 80% ifikapo 2040

Inatarajiwa kuwa uzalishaji wa plastiki utaongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2060.
Inatarajiwa kuwa uzalishaji wa plastiki utaongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2060.Picha: Aurelien Morissard/AP/picture alliance

Uchafu wa plastiki mawinguni na kwenye maziwa ya kina mama

Uchafuzi wa plastiki unapatikana kila mahali, hivi kwamba chembechembe zao zimepatikana hadi kwenye mawingu, kwenye mifereji ya kina kabisa baharini na hata kwenye maziwa ya kina mama wanaonyonyesha.

Japo karibu kila mtu anakubali kuwa uchafuzi wa plastiki ni tatizo, maelewano kuhusu jinsi ya kulitatua, yamesalia kuwa machache.

Mnamo mwaka 2019, ulimwengu ulizalisha karibu tani milioni 460 za plastiki, takwimu ambayo imeongezeka mara mbili tangu mwaka 2000. Hiyo ni kulingana na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo.

Ikiwa hatua mahususi hazitachukuliwa kudhibiti hali, inatarajiwa kuwa uzalishaji wa plastiki utaongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2060.

Mkutano wa Busan unaojadili mkataba wa kukabili uchafuzi wa plastiki, ulijiri saa chache baada ya ule uliokumbwa na vuta nikuvute wa COP29 kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kule Baku kukamilika, ambapo wajumbe hawakuridhishwa na kiasi cha ufadhili uliofikiwa kukabili athari za tabia nchi katika mataifa masikini.

(Vyanzo: AFPE, APTN)