Mfumo wa afya ya umma Kongo uko kiwango kibaya: WHO
1 Julai 2023Matangazo
Kulingana na taarifa ya shirika hilo iliyotolewa jana Ijumaa, ongezeko la machafuko na ukosefu wa usalama vinazidi kuiathiri afya ya umma.
Taarifa ya shirika la afya duniani imesema, mfumo wa huduma za afya na rasilimali kwenye taifa hilo ziko katika shinikizo kubwa kutokana na kuzuka kwa magonjwa kama vile homa ya manjano, kipindupindu na Malaria yanayozidi kuongezeka kutokana na majanga ya asili.
Tangu mwezi Desemba mwaka uliopita kumekuwa na takribani visa 25,000 vya kipindupindu, visa 136,000 vya surua na vifo 2,000 vilivyoripotiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kwa sasa, WHO inahitaji dola milioni 174 za kimarekani ili kutoa msaada wa huduma za afya nchini humo, hata hivyo limefanikiwa kupata dola milioni 23 pekee.