Mfumo wa afya wa Afghanistan katika hatari ya kuporomoka
16 Desemba 2021Mafuta ya dizeli yanayohitajika kwenye mashine ya kuzalisha oxygeni kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 yamekwisha.
Dazeni kadhaa za dawa vilevile hazipo. Madaktari pamoja na wahudumu wa afya pia hawajalipwa mishahara yao kwa miezi kadhaa. Japo wanavumilia na kuwahudumia wagonjwa, hawawezi kuyakidhi mahitaji yao ya kila siku nyumbani.
Hayo ndiyo masaibu yanayoikumba hospitali inayoendeshwa kwa ushirkiano kati ya Afghanistan na Japan inayowahudumia wagonjwa wa maradhi ya kuambukiza. Ndiyo hospitali pekee inayoshughulikia wagonjwa wa COVID-19 mjini Kabul, mji ulio na zaidi ya wakaazi milioni 4.
Japo hali kuhusu maambukizi ya virusi vya corona ilipungua miezi michache iliyopita, kwa sasa hali ya hospitali ndiyo ipo taabani zaidi.
Masaibu yake ni ishara ya utata unaoukumba mfumo wa afya wa Afghanistan ambao uko katika hatari ya kuporomoka. Mfumo unaofanya kazi tu kwa kutegemea wahisani au mashirika ya misaada.
Daktari Ahmad Fatah Habibyar ambaye ni meneja wa mipango katika hospitali hiyo amesema wanakabiliwa na shida nyingi akitaja hali ya kushindwa kuwalipa wafanyakazi wao kwa muda wa miezi mitatu sasa,upungufu wa vifaa vya matibabu ikiwemo dawa na vilevile ukosefu wa chakula.
”Baadhi ya wafanyakazi wetu wanakumbwa na hali ngumu kifedha hivi kwamba wamelazimika kuuza samani zao ndipo waweze kuyakidhi mahitaji yao,” amesema Habibyar.
"Gesi ya oksijeni ni suala tete mno kwa sababu mitambo yetu yaani majenereta yamekwama kwa sababu hatuna dizeli, na hayajafanya kazi kwa miezi kadhaa sasa,” amesema daktari Habibyar.
UN: Afganistan inakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa
Hayo yanajiri wakati ambapo madaktari wanahofia kutakuwa na ongezeko la maambukizi kutokana na aina mpya ya kirusi cha corona omicron.
Daktari Shereen Agha mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni mkuu wa idara ya kuwahudumia wagonjwa mahututi amesema bila ya misaada kutoka nje, basi hawataweza kushughulikia maambukizi kutokana na Omicron.
Kulingana na daktari Agha, hospital hiyo haina vitu vya msingi mfano glovu za madaktari na wahudumu kuvaa wanapowahudumia wagonjwa. Hata magari yao mawili ya kusafirisha wagonjwa hayafanyi kazi kwa sababu ya ukosefu wa mafuta.
Serikali ya awali iliingia kwenye makubaliano na shirika la misaada la Uholanzi HealthNet TPO ili liweze kuisimamia hospitali hiyo. Lakini makubaliano hayo yalimalizika mwezi Novemba na yalifadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo sawa na taasisi nyingine za kimataifa zilisitisha malipo kwa serikali mpya ya Taliban nchini Afghanistan.
Kundi la Taliban lilipochukua usukani mnamo mwezi Agosti, jumuiya ya kimataifa iliondoa ufadhili wao wa mabilioni ya dola nchini Afghanistan. Katika nchi ambayo inategemea pakubwa ufadhili wa kigeni, athari imekuwa mbaya zaidi.
Serikali ya Taliban inaitaka jamii ya kimataifa kulegeza vikwazo na iachilie mali ya Afghanistan ambazo zimezuiwa katika mabenki ya nje, ili iweze kuwalipa wafanyakazi wake mishahara.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu hali ya njaa nchini humo mnamo wakati asilimia 22 ya idadi jumla ya wananchi milioni 38 wakikenuliwa meno na njaa.
Katika miezi minne iliyopita, hospitali hiyo imesema imepokea watu 3,000 wanaokabiliwa na utapiamlo.
(AFPE)