1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfanyabiashara tajiri aliyetekwa hajapatikana: Polisi

Hawa Bigoga11 Oktoba 2018

Polisi nchini Tanzania imesema kuwa bado mfanyabiashara na tajiri mashuhuri barani Afrika Mohammed Dewj aliyetekwa nyara mapema leo hajapatikana.

https://p.dw.com/p/36NNr
Tansania Mohammed Dewji, Geschäftsmann
Picha: Getty Images/AFP/K. Said

Wakati familia ya mfanyabiashara mashuhuri barani Afrika Mohammed Dewj aliyetekwa nyara alfajiri ya leo jijini Dar es Salaam, ikiwa haijatoa tamko lolote, polisi mjini humo imesema kuwa suala la uchunguzi lipo mikononi mwao na bado hajapatikana kama taarifa zinavyosambaa.

Hapo awali habari zilisambaa kuwa mfanyabiashara huyo amepatikana katika fukwe za coco jambo ambalo limekanushwa vikali na jeshi la polisi mchana huu walipozungumza na waandishi wa habari na kutoa wito kwa raia kuhakikisha wanatoa taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa bilionea huyo kijana barani Afrika.

Kamanda wa kanda maalum Lazaro Mambosasa amewaambia wanahabari kuwa, hakuna taarifa rasmi za kupatikana kijana huyo na mfanyabiashara ambae ametekwa na watu wenye asili ya kizungu, wala wahusika waliotekeleza tukio hilo hawajapatikana.

Aidha jeshi la polisi limesema linaendelea na uchunguzi kwa mikoa yote ya kipolisi ya jiji la dare s salaam huku idadi ya wahojiwa ikiongezeka.

Utekaji wa Mohammed Dewj wazusha sintofahamu

Polisi waendelea na uchunguzi kuhusu kutekwa kwa Mohammed dewj
Polisi waendelea na uchunguzi kuhusu kutekwa kwa Mohammed dewjPicha: DW/S. Khamis

Kutekwa kwa Dewj ambae anatajwa kumiliki asilimia arobaini na tisa ya hisa katika klabu kongwe ya mpira wa miguu ya Simba kumeacha hali ya sintofahamu kwa wanachama wa klabu hiyo ambapo msemaji wa simba Haji Manara anawataka kuwa watulivu wakati vyombo vya usalama vikiendelea kufanya kazi yake.

Mohamed Dewji ni mfanyabiashara mashuhuri si tu Tanzania, bali Afrika na ni mkurugenzi mtendaji wa bishara nyingi chini ya mwavuli wa kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd, zilizoanzishwa na baba yake, Gulam Dewji.

Biashara hizo zinahusisha viwanda vya kusindika nafaka kama ngano na mahindi pamoja na viwanda vya vinywaji baridi mara kadhaa ametajwa katika Jarida maarufu la Forbes kama mmoja wa wafanyabiashara wakubwa Afrika.

Tukio hili la kutekwa kwake limeacha hali ya wasiwasi miongoni mwa watanzania hasa ikizingatiwa kuwa, eneo la Oysterbay lilipotokea tukio hilo ni makazi ya watu mashuhuri na mabwanyenye wakiwemo viongozi mbalimbali wa serikali,viongozi wastaafu na hata mabalozi wa nchi mbalimbali.

Mhariri: Yusuf Saumu