1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Uhispania akemea kura ya kujitenga Catalonia

4 Oktoba 2017

Katika mzozo wa jimbo la Catalonia linalotaka kujitenga na Uhispania Mfalme Felipe VI amewaita viongozi wa jimbo hilo watu wanaoligawa taifa. Kauli yake lakini haikuwafanya viongozi hao kulegeza kamba.

https://p.dw.com/p/2lArJ
Mfalme Felipe wa Uhispania
Picha: Reuters/F.Gomez

Hotuba ya Mfalme Felipe VI ilikuwa na lengo la kutuliza mgogoro huo wa kisiasa, mkubwa zaidi kuikumba Uhispania kwa miongo kadhaa, lakini badala yake inaweza kuzidisha mvutano. Mfalme aliitoa hotuba hiyo baada ya maandamano yaliyowahusisha maelfu ya watu wa Catalan, wakilaani ukatili uliofanywa na polisi dhidi ya watu waliojitokeza kupiga kura ya maoni kuhusu uhuru wa jimbo hilo, ambayo kwa mujibu wa serikali na mahakama haikuwa halali.

Katika hotuba yake mfalme Felipe hakuwa na sauti yake ya utulivu, bali aliwashutumu viongozi wanaoongoza harakati za kujitenga, akisema wamekiuka sheria. "Wamevunja msingi wa kila sheria ya nchi na kutishia utengamano wa jamii ya Catalonia, na kuigawa jamii hiyo. Leo hii, Catalonia imepasuka na inakabiliwa na changamoto. Viongozi hao wamejidanganya kuhusu mshikamano wa wahispania, na kwa vitendo vya visivyo vya kuwajibika, wanahatarisha usalama wa kijamii na kiuchumi, sio tu kwa Catalonia, bali kwa Uhispania nzima."

Idadi kubwa ya waliopiga kura wanataka Catalonia ijitenge na kuwa taifa huru
Idadi kubwa ya waliopiga kura wanataka Catalonia ijitenge na kuwa taifa huruPicha: Getty Images/AFP/P.-P. Marcou

Watu wa Catalonia waliokuwa wakiitazama hotuba hiyo ya mfalme hawakupendezwa na kauli yake. Domingo Gutierrez, mzee mwenye umri wa miaka 61 aliyesikiliza na wenzake katika baa mjini Barcelona, amesema hotuba ya mfalme ilikuwa aibu tupu. "Kwa kushindwa kusema chochote kuhusu mamia ya watu waliojeruhiwa na polisi, alichofanya ni kuongeza mafuta kwenye moto", alisema Gutierrez.

Kiongozi wa Catalonia ashikilia msimamo

Mcatalan mwingine aliyejitambulisha kama Gelardo, alisema hotuba ya mfalme haikuwalenga wao. "Aliyoyasema mfalme hayahusu hali wanayoishuhudia mitaani watu wa Barcelona na Catalonia. Analenga hadhara ya Uhispania. Hatujihisi kama amezungumza na sisi wala anatujali. Hakuna alichokisema ambacho kinaweza kutupa njia mbadala kwa maandamano ambayo kwa miaka kadhaa yamekuwa yakiendelea."

Kiongozi wa mamlaka ya ndani ya jimbo la Catalonia Carles Puchdemont, ambaye anashutumiwa vikali ya serikali kuchochea chuki na mgawanyiko, ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC kwamba haitachukua muda mrefu kwa kujitangazia uhuru. ''Tutajitangazia uhuru katika muda wa masaa 48 baada ya kura zote kuhesabiwa na matokeo kuwekwa hadharani," amesema Puigdemont, akiongezea kwamba shughuli hiyo itakamilika mwishoni mwa juma hili, au mwanzoni mwa juma lijalo.

Puigdemont amesema kwa sasa hawana mawasiliano yoyote na serikali kuu mjini Madrid, na alipoulizwa wanajiandaa kufanya nini ikiwa serikali kuu itaingilia kati kuchukuwa hatamu za utawala jimboni Catalonia, alijibu kuwa hili litakuwa kosa kubwa, ambalo litabadilisha kila kitu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri: Elizabeth Shoo