1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Saudi Arabia azungumza na Erdogan

Mtullya Abdu 12 Aprili 2016

Mfalme Salman wa Saudi Arabia yuko nchini Uturuki kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa shirika la ushirikiano la nchi za kiislamu OIC. Salman anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Erdogan wa Uturuki.

https://p.dw.com/p/1ITjE
Mfalme Salman wa Saudi Arabia
Picha: Getty Images/AFP/S.Loeb

Mfalme wa Saudi Arabia, Salman Bin Abdel- Aziz, aliwasili mjini Ankara Jumatatu kuanza ziara nchini Uturuki yenye lengo la kuimarisha uhusiano ambao tayari ni wa ndani baina ya nchi yake na Uturuki.

Mfalme Salman tayari amekutana na mwenyeji wake, Rais Erdogan na kuzungumzia juu ya mgororo wa nchini Syria na juu ya kupambana na magaidi wanaojiita Dola la kiislamu.

Afikia kwenye hoteli ya kifahari

Vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti kuwa mtawala huyo wa Saudi Arabia amefikia kwenye hoteli yenye ukubwa wa mita za mraba 4,850 mjini Ankara. Hoteli hiyo ina madirisha yenye vihami dhidi ya risasi na milango iliyojengwa kwa saruji inayoweza kuzuia mabomu.

Mfalme wa Saudi Arabia aliwasili nchini Uturuki kutokea Misri. Ujumbe wa watu mia tatu ulitangulia mjini Ankara kuratibisha mambo ya malazi,itifaki na usalama wa mfalme.

Saudi Arabia na Uturuki zimeujenga tena uhusiano wa ndani baina yao baada ya uhusiano huo kuharibika kutokana na dhima ya Saudi Arabia katika kuondolewa madarakani kwa aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi wa Misri mnamo mwaka wa 2013. Mursi alikuwa mshirika mkubwa wa Uturuki.

Uturuki na Saudi Arabia zimekuwa zinashirikiana katika vita vya nchini Syria dhidi ya Rais Bashar-al Assad. Katika vita hivyo nchi hizo mbili zimekuwa zinawaunga mkono waasi wanaowania kumwondoa madarakani Rais Assad.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/J. Roberts

Mnamo mwezi wa Februari ndege za kijeshi za Saudi Arabia ziliwasili kwenye kituo cha Incirlik kusini mwa Uturuki ili kushiriki katika kuwashambulia magaidi wanaojiita dola la Kiislamu nchini Syria.

Hapo Alhamisi, Mfalme wa Saudi Arabia ataanza kushiriki kwenye mkutano wa kilele wa shirika la ushirikiano la nchi 57 za kiislamu, OIC. Wajumbe kwenye mkutano huo wa siku mbili watalijadili suala la Wapalestina, migogoro baina ya nchi wanachama na njia za kupambana na ugaidi.

Salman avishwa medali ya heshima

Mkutano huo wa 13 utafanyika katika muktadha wa migogoro katika nchi kadhaa za Kiislamu, ikiwa pamoja na Yemen na Syria. Wakuu wa serikali na viongozi wa nchi zaidi ya 30 wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano huo chini ya uenyekiti wa Rais wa Uturuki Erdogan.

Maafisa wa shirika la ushirikiano la nchi za Kiislamu wameipitisha ajenda ya mkutano na watafuatiwa na mkutano wa matayarisho wa mawaziri wa mambo ya nje hapo kesho na Jumatano. Wakuu wa serikali na viongozi wa nchi watakutana kwa siku mbili kuanzia Alhamisi.

Wakati huo huo Rais Tayyip Erdogan amemtunukia Mfalme Salman medali ya heshima ya juu kabisa ya nchini Uturuki. Rais Erdogan ameeleza kuwa mtawala huyo wa Saudi Arabia amevishwa medali hiyo ya heshima kama ishara ya kuutambua mchango mkubwa alioutoa katika kuendeleza uhusiano wa kirafiki baina ya nchi yake na Uturuki.

Saudi Arabia imeibuka kuwa mshirika mmojawapo muhimu wa Uturuki baada ya kipindi cha mvutano. Mnamo mwaka huu majeshi ya nchi hizo yalifanya mazoezi ya kijeshi ya pamoja na zimekuwa zinajenga mshikamano thabiti wa kijeshi.

Mwandishi: Mtullya Abdu/ape,rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga