1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Afrika Kusini aanza kifungo leo

Admin.WagnerD31 Desemba 2015

Mfalme wa Afrika Kusini, Buyelekhaya Dalindyebo, kutoka kabila la Rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Nelson Mandela la Abu Thembu leo ameanza kutumikia kifungo cha miaka 12 gerezani

https://p.dw.com/p/1HWYx
Südafrika Flagge

Mfalme Buyelekhaya Dalindyebo ameripoti katika gereza la Mthatha Mashariki mwa mkoa wa Cape jana usiku, mara tu baada ya kushindwa jitihada zake za miezi 11 za kukwepa kufungwa jela kwa kupata msamaha wa rais.

Charles Nwaila, Mkurugenzi wa idara ya mambo ya mila na desturi amesema hii ni kesi ya mtu mmoja tu na haitarajiwi kubadilisha mahusiano baina ya katiba ya nchi na taasisi ya uongozi wa kifalme nchini humo.

Aliongeza kusema, somo la kujifunza kutokana na kesi hiyo ni kwamba lazima kuwe na uangalifu mzuri wa kufuata sheria bila ya kujali cheo cha anayeshutumiwa.

Mnamo mwaka 2009, mfalme huyo alikutikana na hatia ya mauaji, kuchoma mali za watu kwa makusudi, na makosa mengine aliyoyafanya zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Mfalme Dalindyebo alihukumiwa kifungo cha miaka 15 mwaka 2009, lakini mwezi Oktoba mwaka huu, Mahakama Kuu ilimfutia shutuma za mauaji na kupunguza kifungo chake hadi miaka 12 baada ya kukata rufaa.

Wiki hii mfalme huyo alijaribu kutaka kuongeza muda wa kuwa nje kwa dhamana, lakini hakimu wa Mahakama Kuu wa mji wa Mthatha alilitupilia mbali ombi hilo.

Hatia zilompeleka jela

Mfalme huyo anatarajiwa kutumikia kifungo chake katika gereza la Wellington, nje kidogo ya mji wa Mthatha. Mfalme Dalindyebo anayejitaja mwenyewe kuwa ni mvutaji mzuri wa bangi alikutikana na hatia za kuzitia moto nyumba za baadhi ya wapangaji wake waliokataa kuhama makaazi yao.

Halikadhalika alikutikana na hatia za kuwashambulia vijana watatu hadharani baada ya kupigwa vibaya na watu wake, sio hayo tu pia amekutikana na hatia ya kumteka nyara mke na watoto wa mmoja wa wapinzani wake.

Mahakama Kuu imehitimisha hukumu yake kwa kusema mfalme Dalindyebo alitawala kwa kutumia hofu na vitisho, na kwamba vitendo vyake vinasikitisha zaidi kwasababu walioathirika na uongozi wake ni watu wanaoishi vijijini katika hali ya umasikini mkubwa.

Mfalme Dalindyebo aliingia madarakani mwaka 1989 na ni mmoja wa wafalme 10 wa kikabila ambao majukumu yao ni kuhudhuria sherehe za kimila pamoja na kusimama kama wapatanishi wakati wa migogoro ya vijijini .

Baraza la Ufalme wa AbaThembu sasa litajadili kama nafasi ya mfalme Dalindyebo itazibwa kwa muda mrefu ama mfupi. Na iwapo Baraza hilo litaamua kumuweka mfalme mpya wa muda mrefu, basi litahitaji kupata idhini ya Rais Jacob Zuma, ambaye atampokonya Dalindyebo cheti cha utambulisho kama mfalme na kumpa mfalme mpya atakaeteuliwa na baraza hilo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman