Mexico yaituliza Brazil
18 Juni 2014Baada ya mlinda lango wa Mexico Ochoa kuokoa nafasi nne muhimu katika mechi hiyo iliyokamilika kwa sare tasa, wengi walijitokeza kumpa pongezi kwa ustadi wake.
Mmoja wao ni aliyekuwa mlinda lango nambari moja wa Ujerumani Oliver Kahn aliyesema kuwa “huo ndio mchezo bora zaidi uliowahi kuonyeshwa na mlinda lango katika dimba hili kufikia sasa”.
Julio Ceaser katika lango la Brazil vile vile alizuia nafasi kadhaa muhimu kutoka kwa upande wa Mexico, lakini kazi aliyofanya Ochoa ilikuwa ya kuvutia sana, na hasa kwa sababu Brazil ndio iliyokuwa na nafasi chingi nzima za kutikisa wavu.
Neymar ambaye anatafuta goli lake la tatu katika dimba hilo, ni mmoja wa wachezaji walionyimwa goli na miujiza ya Ochoa katika kipindi cha kwanza. Neymar aliruka juu hewani na kupiga kichwa safi kutoka kwa krosi iliyochongwa na Dani Alves, lakini kipa wa Mexico akapangua.
Hector Herrera alikuwa na nafasi mbili nzuri za kuwafungia Mexico kwa kusukuma makombora ya mbali. Safu ya ulinzi ya Mexico yenye mabeki watano ilifanya kazi nzuri ya kuwazuia Wabrazil.
Mchuano huo ulikuwa wa kusisimua isipokuwa tu magoli. Kiungo mkabaji wa Brazil Luiz Gustavo alisema baadaye kuwa ulikuwa mpambano wa kasi na mgumu. Timu zote zilikuwa na nafasi za kufunga, na ilikuwa mechi nzuri, na sasa wanastahili tujiandaa kwa mechi ya mwisho ya makundi.
Mexico na Brazil sasa zina pointi nne kila mmoja wakati zikiingia katika mechi za mwisho za kundi A, na zote zinapigia upatu kufuzu katika duru ya mwondowano. Sasa ni zamu ya Croatia na Cameroon pia zina nafasi za kujaribu kujipenyeza kama zitashinda mchuano wao Alhamisi katika joto kali la Manaus.
Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Abdul-Rahman