1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meta kuchunguzwa juu ya usalama wa watoto mtandaoni

Saleh Mwanamilongo
17 Mei 2024

Umoja wa Ulaya umeanzisha uchunguzi mpya dhidi ya mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram kwa madai kwamba mitandao hiyo imeshindwa kuwalinda watoto mtandaoni.

https://p.dw.com/p/4g0w5
Meta-Facebook
Kampuni ya teknolojia ya MetaPicha: Jaap Arriens/NurPhoto/picture alliance

Uchunguzi huo ni hatua ya hivi karibuni ya kuikagua kampuni mama ya Meta kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Kidijitali, DSA, ya mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Na ikiwa ni htua ya kutekeleza kanuni zilizoanza kutumika mwaka jana kwa lengo la kusafisha mitandao ya kijamii na kuwalinda watumiaji wa mitandao.

Mark Zuckerberg
Mark ZuckerbergPicha: Manuel Balce Ceneta/AP/picture alliance

Halmashauri ya Ulaya, chombo kikuu cha utendaji cha Umoja wa Ulaya, imeibua wasiwasi kwamba mifumo ya algorithm inayotumiwa na mitandao yaFacebookna Instagram kupendekeza maudhui kama video na machapisho inaweza kutumia udhaifu na udhoefu wa watoto. Na hivyo kuchochea tabia ya uraibu kwa watoto hao. Umoja wa Ulaya pia una wasiwasi kwamba mifumo hii inaweza kuimarisha kile ulichokiita "shimo la sungura" : inayomaanisha athari ambayo inaongoza watumiaji kwenye maudhui yanayosumbua.

Halmashauri ya EU pia inaangalia matumizi ya Metaya zana za uthibitishaji wa umri ili kuzuia watoto kufikia mitandao ya Facebook au Instagram, au watoto hao kuonyeshwa maudhui yasiyofaa. Mitandao ya kijamii inahitaji watumiaji kuwa angalau na umri wa miaka 13 kufungua akaunti. Pia inaangalia kwa undani ikiwa kampuni ya Meta inatii sheria za DSA zinazohitaji kiwango cha juu cha faragha, usalama na usalama kwa watoto.

Mkurugenzi wa TikTok Shou Zi Chew
Mkurugenzi wa TikTok Shou Zi ChewPicha: Manuel Balce Ceneta/AP/picture alliance

Kwenye taarifa, Kampuni ya Meta alisema inataka vijana wawe salama, na uzoefu unaolingana na umri wao mtandaoni.Ulaya kukabiliana na teknolojia ya akili bandia

Kwa hivyo Meta imesema imetumia muongo mmoja kutengeneza zana zaidi ya Hamsini pamoja na sera iliyoundwa kuwalinda watoto. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa hiyo ni changamoto ambayo tasnia nzima inakabili, na Meta inasubiri kuzungumzia kwa undani kazi yake na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Hizi ni kesi za hivi karibuni zaidi za EU chini ya sheria ya huduma za kidigitali zinazolenga ulinzi wa mtoto. Sheria hizo zinahitaji mitandao ya kijamii kuweka hatua kali ili kulinda watoto. Halmashauri ya EU ilifungua chunguzi mbili tofauti mapema mwaka huu dhidi ya mtandao wa kijamii wa TikTok juu ya wasiwasi kuhusu maudhui hatari kwa watoto.

Vigezo vya kuzingatia unapoomba au unapokubali urafiki mitandaoni

Thierry Breton, Kamishna wa EU nayehusika na soko la ndani amesema hawana uhakika kuwa Meta imefanya vya kutosha kufuata sheria na majukumu ya sheria ya huduma za kidigitali. Na vilevile kupunguza athari mbaya kwa afya ya kimwili na kiakili ya vijana wa Ulaya kwenye mitandao yake Facebook na Instagram.

Uchunguzi huo uliotangazwa na EU sio wa kwanza dhidi ya Facebook na Instagram. Tayari mitandao hiyo ilichunguzwa juu ya wasiwasi kwamba haifanyi vya kutosha kukomesha taarifa ghushi za kigeni kabla ya uchaguzi wa EU mwezi ujao.

Mtandao wa kijamii wa X , zamani Twitter, na tovuti ya biashara ya mtandaoni ya AliExpress pia zimechunguzwa kufahamu ikiwa zimefuata sheria za Umoja wa Ulaya. Hakuna tarehe ya mwisho kwa uchunguzi huo kukamilika. Na ikiwa makampuni hayo yatakutwa na hatia, yanaweza kutozwa faini ya hadi asilimia sita ya jumla ya pato lao la mwaka.