Messi atabaki Barcelona; hali inayoleta utata mpya
5 Septemba 2020Jogoo huyo nyota wa Argentina alitangaza siku ya Ijumaa kuwa amelazimika kubakia Barcelona, akidai ni baada ya rais wa klabu hiyo Josep Maria bartomeu kukiuka kauli yake kumwachia aondoke.
Imekuja siku 10 baada ya hali ya wasi wasi na mvutano wa mtikisiko wa taarifa yake kwa njia ya fax iliieleza Barcelona kwamba anataka kuondoka.
Lakini wakati wachezaji wengine ikiwa ni pamoja na Jordi Alba na Philippe Coutinho waliwasili kwa ajili ya mazowezi hayo, Messi alishindwa kujitokeza katika uwanja wa mazowezi wa Joan Gamper kwa ajili ya mazowezi ambayo yameanza leo asubuhi.(05.09.2020)
Jumapili iliyopita Messi kwa makusudi mazima aliepa kufanyiwa vipimo vya lazima vya virusi vya corona ambavyo wachezaji wote wa barcelona wanalazimika kufanyiwa. Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Messi ni lazima kwanza apate uthibitisho kuwa hana maambukizi ya COVID-19 na anaweza kurejea katika kikosi hicho huenda Jumatatu.
Anaweza baada ya hapo kuingia katika mipango ya mchezo wa kwanza wa kocha mpya Ronald Koeman, mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya daraja la tatu Nastic hapo Septemba 12.
Mazungumzo na vilabu vingine
Lionel Messi anabakia Barcelona lakini kwa muda gani? Messi anaweza kufanya mazungumzo na timu nyingine kuanzia Januari mosi na kuondoka katika klabu hiyo majira ya joto mwakani, wakati mkataba wake utakapomalizika na mara hii ataondoka bila kulipiwa fedha za uhamisho. Hadi wakati huo , Barca inabidi kutafuta njia ya kumrejesha kundini mchezaji wake huyo nyota, ambaye hataki tena kucheza katika timu hiyo.
Tangazo lake ambalo lilikuwa na viashiria vya uchungu siku ya Ijumaa halikupokelewa kwa sherehe, hata miongoni mwa mashabiki, wengi wao waliunga mkono uamuzi wake wa kuondoka, wakipata ahueni kidogo katika wazo lake la kutafuta mafanikio sehemu nyingine.
Kulikuwa na ukimya pia kutoka kwa wachezaji wenzake, hakuna aliyeonesha kumpa uungwaji mkono hadharani ambao Luis Suarez na Carles Puyol walitoa wakati Messi alipoiambia Barca anataka kuondoka.
Hata klabu hiyo pia ilionekana haina hakika juu ya vipi kuangalia tamko la Messi. Ilichukua karibu masaa matatu kabla ya picha ya Messi kuingia katika jukwaa lake la mitandao ya kijamii, kukiwa na maneno chanya tu ambayo alizungumza wakati wa mahojiano yake hapo mapema, sio kupitia vyombo rasmi vya klabu hiyo, lakini kwa njia ya Goal.
Shingo upande
"Nitatoa uwezo wangu wote. Mapenzi yangu kwa Barca hayatabadilika", ilisomeka.
Lakini hata iwapo nia ya Messi ni safi, vipi hataweza kubadilika kutokana na hili ? Uchungu wake ulionekana wazi na hisia zake zilikuwa wazi.
Kama rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu hakusimama katika njia ya Messi, alikuwa ameondoka, huenda kwa hivi sasa angekuwa ana sare ya Manchester City na kufanya mazowezi katika uwanja wa Etihad.
Badala yake amelazimishwa kubaki kinyume na matakwa yake na kubakia kama sehemu ya mradi ambao hana imani nao tena.
Nabaki hapa kwasababu rais amesema njia pekee ya mimi kuondoka ni kulipwaeuro milioni 700 katika kifungu cha kuachana, ambazo ni vigumu kulipwa, ama njia nyingine ni kwenda mahakamani," Messi alisema.