1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Ugiriki kuimarisha mshikamano

10 Januari 2019

Mamlaka nchini Ugiriki zimepiga marufuku maandamano katika eneo kubwa la katikati mwa mji mkuu Athens na kuzifunga barabara na vituo vya treni za chini ya ardhi wakati Kansela Angela Merkel akiwasili mjini humo

https://p.dw.com/p/3BJy6
EU Gipfel in Brüssel Angela Merkel mit Alexis Tsipras
Picha: picture-alliance/abaca/D. Aydemir

Karibu polisi 2,000, helikopta ya polisi na ndege zisizoruka na rubani zitatumiwa wakati wa ziara hiyo, itakayokamilika kesho Ijumaa mchana.

Ujerumani ndiyo iliyokuwa mchangiaji mkubwa kabisa kwa mfuko wa kimataifa wa fedha za uokozi zilizotolewa katika awamu tatu ambazo Ugiriki ilipokea tangu mwaka wa 2010 wakati ikikabiliwa na mgogoro mkali wa kifedha ambapo nchi hiyo ilikaribia kujiondoa katika kanda ya sarafu ya euro.

Ujerumani pia ilionekana kuwa mmoja wa nchi zilizoishinikiza nchi hiyo kutekeleza hatua kali za kubana matumizi, ikiwa ni pamoja na kupandisha kodi na kupunguza pensheni na mishahara, ilizowekewa nchi hiyo ili nayo ipokee mikopo ya uokozi.

Merkel na Tsipras wamekutana ana kwa ana mara nyingine katika miaka iliyopita, lakini hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kansela huyo wa Ujerumani kuzuru Athens chini ya serikali ya Tsipras. Aliingia madarakani Januari 2015 baada ya kuendesha kampeni kali ya kupinga mipango ya uokozi wa Umoja wa Ulaya na kumpinga Merkel, ambapo wakati mmoja alitangaza kwenye hotuba yake ya kampeni kabla ya uchaguzi wa Ulaya: kuwa "Rudi kwenu, Bibi Merkel!”

Europa Finanzen l Steuer auf Finanztransaktionen l Europäische Zentralbank Euro-Skulptur
Ugiriki ilipewa mkopo wa uokozi kwa awamu tatuPicha: Getty Images/AFP/D. Roland

Mahusiano yameimarika tangu wakati huo, na Tsipras akaachana na msimamo wake wa kupinga masharti ya kubana matumizi, kwa kuyatekeleza mageuzi ambayo wakopeshaji wa Ugiriki waliiambia iyafanye.

Ugiriki ilishuhudia uchumi wake ukidorora kwa robo wakati wa mgogoro huo, ambapo ukosefu wa ajira ulipanda hadi asilimia 28, na asilimia 58 kwa vijana. Kiwango cha wasio na kazi kimepungua tangu wakati huo hadi chini kidogo ya asilimia 19.

Merkel amesema katika taarifa iliyochapishwa na gazeti la Athens kabla ya ziara yake anafamu kuwa miaka michache iliyopita ilikuwa migumu sana kwa watu wengi nchini Ugiriki.

Ameongeza kuwa Ulaya ilionyesha mshikimano wake kwa kuwa na mfuko wa fedha za uokozi zilizotolewa kwa awamu tatu na kuisaidia Ugiriki katika mchakato wake wa mageuzi kuelekea uimara wake wa kifedha na kiuchumi, mchakato ambao amesema bila shaka ulikuwa mgumu sana.

Ugiriki ilitoka katika awamu ya tatu na ya mwisho ya mpango wa uokozi mwezi Agosti mwaka jana, lakini uchumi wake utaendelea kuwa chini ya uchunguzi mkali na imeahidi kufanya mageuzi Zaidi ili kuhakikisha kuwa fedha zake zinabaki kwenye mkondo sahihi.

Kando na mgogoro wa kifedha, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili uhamiaji, suala ambalo misimamo ya Tsipras na Merkel imekaribiana kwa kiasi, pamoja na makubaliano ya jina ambalo Ugiriki ilifanya na Macedonia.

Chini ya makabaliano hayo yaliyofikiwa mwaka jana, jamhuri hiyo ya zamani ya Yugoslavia itapewa jina la Macedonia Kaskazini nayo Ugiriki isitishe pingamizi lake kwa nchi hiyo kujiunga na Jumuiya ya Kujihami NATO na kisha Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga