1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Ujerumani imejitahidi kupambana na kirusi cha corona

7 Oktoba 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametetea rekodi iliyowekwa na serikali yake wakati wa janga la virusi vya corona na kuwaeleza wabunge kwamba Ujerumani imefanya vyema ikilinganishwa na mataifa mengine ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/3jYav
Berlin | Angela Merkel bei Verleihung des Integrationspreises
Picha: Kay Nietfeld/Reuters

Kwenye mjadala wa bajeti wa bunge la Ujerumani, Bundestag, chama cha Mbadala wa Ujerumani cha AfD, ambacho ni kikubwa zaidi cha upinzani bungeni, kimemtuhumu kansela Angela Merkel kwa kuutumia mzozo wa virusi vya corona kama kisingizio cha kuzitumia fedha za kodi za wananchi kuhamasisha kile ilichokielezea kama "ujamaa wa corona”.

Merkel ameyakana madai hayo, akisisitiza kwamba licha ya kuunganisha pamoja mafungu makubwa ya uokozi na kuondoa kanuni zake za awali za kukopa, Ujerumani imeendelea kuwa na kiwango cha chini cha uwiano wa deni la umma ikilinganishwa na kundi la mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi la G7.

Ujerumani kama ilivyo kwa mataifa mengine jirani ya Ulaya imeshuhudia ongezeko la visa vya maambikizi ya virusi vya corona katika wiki za karibuni. Maafisa wamechapisha takwimu siku ya Jumatano zinazoonyesha visa vipya 1,798 kote nchini humo katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, na kufanya idadi jumla ya maambukizi kufikia 289,219 tangu kisa cha kwanza kilipotangazwa. Ujerumani pia ina karibu vifo 9,500 vilivyothibitishwa kusababishwa na COVID 19, ambayo ni moja ya nne, ya idadi jumla ya Uingereza ama Italia.

Berlin | Pressekonferenz zu Pflege und Corona: Jens Spahn
Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Kiongozi huyo wa muda mrefu, ambaye tayari amethibitsha kutogombea kwa awamu ya tano, kabla ya kumaliza hotuba yake mbele ya bunge aliugeukia umma na kuwaambia watu kufuata kanuni zilizowekwa katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Alinukuliwa akisema, "hatujafikia mwisho wa janga hili.” Na kuongeza kuwa Ujerumani inakabiliwa na nyakati mgumu katika siku za usoni za baridi na vuli. Amesema, kanuni za kukaa mbalimbali na usafi haziwahusu tu watu wa kundi linalitajwa kama liko hatarini, bali zinamhusu kila mmoja.

USA Trump verlässt Krankenhaus
Rais Trump baada ya kurejea Ikulu anakoendelea kujiuguzaPicha: Erin Scott/Reuters

Katika hatua nyingine nchini Marekani, rais Donald Trump ametangaza kusitisha majadiliano kuhusiana na raundi nyingine ya fedha za msaada wa kunusuru uchumi nchini humo. Trump aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter mapema kwamba anasitisha mazungumzo hayo hadi baada ya uchaguzi.

Tangazo hilo linakuja baada ya mwenyekiti wa Benki kuu nchini humo Jerome Powell kuliomba bunge kuja na msaada zaidi, akisema kwamba msaada finyu hautabadilisha chochote zaidi ya kulipeleka taifa hilo kwenye mzozo mkubwa zaidi wa kiuchumi na kuongeza ugumu usio wa lazima.

Trump aliandika kwenye Twitter akimtuhumu spika wa bunge Nancy Pelosi kwamba hakuna na nia njema katika mazungumzo hayo na kuongeza kuwa amemuomba kiongozi wa walio wengi kwenye baraza la seneti Mitch McConnel kuelekeza nguvu zake zote katika mchakato wa kumuidhinisha mteule wake wa mahakama ya juu kabisa nchini humo Amy Coney Barrett kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.SomaUjerumani yarefusha agizo la watu kutokaribiana

Hata hivyo muda mfupi baadae alionekana kubadilisha msimamo na kuandika tena kwenye twitter akiliomba bunge kuidhinisha baadhi ya mafungu ikiwa ni pamoja na bilioni 25 za mashirika ya ndege na bilioni 135 za kusaidia biashara ndogondogo.

Kubadilika huko kwa Trump ambako hakukutarajiwa kunaweza kuwa pigo kwenye mchakato wake wa kuchaguliwa tena katika wakati ambapo serikali yake na kampeni kwa pamoja vikiwa kwenye mvutano. Trump yuko karantini na tafiti za maoni sasa zikimounyesha kuwa nyuma mno ya mpinzani wake Joe Biden wa chama cha Democratic ambaye amekosoa vikali hatua hiyo ya Trump zikiwa zimesalia wiki nne tu kabla ya uchaguzi.