1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: ''Tunatofautiana na Trump kuhusu Korea Kaskazini''

Daniel Gakuba
21 Septemba 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mahojiano maalumu na DW, na kuelezea mtazamo wake kuhusu masuala kadhaa muhimu kimataifa, ukiwemo mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, na pia uchaguzi ujao nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2kOCB
Deutschland wählt DW Interview mit Angela Merkel
Picha: DW

Merkel: Tunatofautiana wazi wazi na Trump kuhusu Korea ya Kaskazini

Katika mahojiano na DW, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza kuwa lazima mzozo wa Korea Kaskazini usuluhishwe kwa njia za kidiplomasia. Na amesema Ujerumani inaweza kuwa msuluhishi katika mzozo huo.

Katika mahojiano hayo, Kansela Merkel ameikosoa hotuba iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Rais Trump alitishia katika hotuba hiyo, kwamba Marekani inaweza kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini.

Kansela Merkel amesema kwamba anapinga vitisho vyovyote. ''Napinga vitisho vya aina zote. Lazima niseme maoni yangu binafsi na ya serikali, ni kwamba suluhisho la kijeshi halifai, tunapendelea juhudi za kidiplomasia. Hili lazima litekelezwe kwa dhati. Kwa maoni yangu, vikwazo na kutekeleza vikwazo hivyo ni jibu sahihi. Kitu kingine zaidi kuhusu Korea Kaskazini nadhani ni makosa. Na ni kwa sababu hiyo tunatofautiana kabisa na rais wa Marekani.'' Amesema Kansela Merkel.

Ujerumani tayari kuwa msuluhishi

Deutschland wählt DW Interview mit Angela Merkel
Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi wa DW, Ines Pohl na Jafaar Abdul KarimPicha: DW

Ujerumani ni miongoni mwa nchi chache ambazo bado zina ubalozi katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, na pia ubalozi wa nchi hiyo mjini Berlin, huku pia ikiwa na mahusiano mema na China, Japan, Korea Kusini na Marekani.

Wakati huo huo, Kansela Merkel amesisitiza utayarifu wa Ujerumani kutoa mchango wake katika kuutafutia suluhisho mzozo wa Korea Kaskazini.

''Ingawa mzozo huo uko mbali nasi kijiografia, bado unaweza kuwa na athari kwetu'', amesema Kansela Angela Merkel katika mahojiano hayo maalumu na DW.

Kansela Merkel amekumbushia mazungumzo ya kuhusu mzozo wa nyuklia ya Iran, ambamo Ujerumani ilishiriki. ''Tunataka majibu ya kidiplomasia, kama tunavyofanya kuhusiana na mgogoro wan Ukraine''. Amesema Merkel, na kuongeza kuwa alimweleza hayo Rais Trump kwa njia ya simu, kabla ya hotuba ya rais huyo katika Umoja wa Mataifa mjini New York.

Uwezekano wa kuwasiliana na Kim Jong-un?

Alipoulizwa kama binafsi anaweza kuwasiliana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, Kansela Merkel amesema, ''Hilo haliko kwenye agenda kwa sasa, sizungumzii uamuzi ambao haujachukuliwa. 

Kansela Angela Merkel amezungumzia pia mvutano uliopo baina ya Uturuki na Ujerumani, akisema, ''Hatutaki kuhamishia matatizo ya Uturuki nchini Ujerumani''.

Na kuhusu chama cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD ambacho kinapigiwa upatu kupata kura nyingi katika uchaguzi wa Septemba 24, Bi Merkel amesema ''kamwe siwezi kufanya kazi na chama hicho''.

Ujerumani haitaki mgogoro na Uturuki

Hivi karibuni, mzozo kati ya Ujerumani na Uturuki umekuwa ukishika kasi, lakini katika mahojiano haya, Kansela Merkel amesema Ujerumani haitaki uhasama na Uturuki. Kinachompa wasiwasi, amesema Kansela Merkel, ni uwezekano kuwa makundi ya Waturuki waishio nchini Ujerumani, yanaweza kuwa yakichunguzana. Amesema Ujerumani haiyataki hayo; ''Tutahakikisha kwamba makundi hayo yote yanaishi kwa amani hapa, bila kudhurika''. Amesema Merkel.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba
Mhariri: Mohammed Khelef