Merkel: Tunahitaji mshikamano kupambana na Corona
19 Machi 2020Katika hotuba ya nadra aliyoitoa kwa taifa kwa njia ya televisheni, Kansela Angela Merkel amesema kila mtu ana jukumu muhimu la kufanya ili kukabiliana na janga la Corona ambalo limesababisha mataifa mengi kufunga miji ili kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Amesema "Hali ilivyo sasa ni mbaya. Tuwe makini na suala hili. Tukiliacha suala la kuunganisha Ujerumani Mashariki na Magharibi au hata vita vya pili vya dunia, Hii ni changamoto kubwa ambayo inategemea sana mshikamano wetu"
Katika muda wa miaka 15 akiwa mamlakani, Kansela huyo amekabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mzozo wa wakimbizi mwaka 2015 na pia suala la Brexit lakini hajawahi kutoa hotuba moja kwa moja isipokuwa tu wakati wa sikukuu za mwaka mpya.
Mamlaka nchini Ujerumani imeamua kufunga shule na kuzuia mikusanyiko ya umma katika siku za hivi karibuni katika hali ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona. Hata hivyo, haijaamuru watu kusalia majumbani kama zilivyofanya Ufaransa, Ubelgiji, Italia na Uhispania.
Wakati huo huo, nchi za magharibi zimekubaliana kutoa karibu dola trilioni moja ili kuunusuru uchumi wa dunia wakati ambapo Italia inaripoti idadi kubwa ya vifo kila siku kutokana na virusi vya Corona.
Jana Jumatano, Italia iliripoti karibu vifo 500 kutokana na Corona, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi kwa siku moja kwa nchi ambazo zimerekodi maambukizi ya virusi hivyo.
Kadhalika Rais Donald Trump wa Marekani ameagiza hatua mpya za kupambana na janga hilo, huku akijitangaza mwenyewe kuwa Rais wa vita kutokana na mlipuko huo.
Wakati hali inaendelea kuwa mbaya barani Ulaya na Marekani, nchini China hali ni tofauti. Alhamisi (19.03.2020) nchi hiyo ya Mashariki mwa Asia haijaripoti maambukizi mapya ya virusi vya Corona kwa mara ya kwanza tangu kutokea kwa mlipuko huo mjini Wuhan mnamo Disemba mwaka uliopita.
Takriban watu milioni 56 katika mkoa wa Hubei na mji mkuu wake Wuhan, walikuwa wamezuiwa kutoka tangu mnamo mwezi Januari lakini sasa mamlaka imeanza kuondoa vikwazo vya usafiri na kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao za kawaida.
Chanzo AFP