1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Trump wakutana

18 Machi 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekutana na rais Donald Trump wamezungumzia masuala ya ushirkiano kati ya Marekani na Ujerumani, migogoro nchini Ukraine, Syria na Libya na pia mapambano dhidi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/2ZSzf
USA Merkel und Trump
Picha: picture alliance/dpa/AP/P. Martinez Monsivais

Viongozi wa mataifa makuu ya Magharibi wamekutana mjini Washington kwa mara ya kwanza kuyazungumzia masuala ya uhusiano baina ya nchi zao, biashara, harakati za kupambana na ugaidi na juu ya kuitatua migogoro ya dunia. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwenyeji wake Rais wa Marekani Donald Trump wamesisitiza umuhimu wa kuiimarisha jumuiya ya kujihami ya NATO. Rais Trump alisema amemsisitizia kansela Merkel kwamba anaiunga mkono kwa uthabiti jumuiya ya NATO. Trump pia alisema kuna umuhimu kwa nchi wanachama kuchangia gharama za ulinzi katika ushirikiano wa jumuiya ya NATO. Rais huyo wa Marekani alisema nchi nyingi hazijalipa michango yao kwa miaka iliyopita na hivyo akalalamika kwamba Marekani haitendewi haki katika hili.

 Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na mgeni wake kansela wa Ujerumani, rais Trump ameitaka kila nchi mwanachama wa jumuiya hiyo ichangie asilimia 2 ya pato lake la taifa kwa ajili ya bajeti ya NATO. Akiijibu kauli ya rais Trump kansela Merkel ameahidi kwamba Ujerumani itautimiza wajibu wake kwa NATO kwa kuchangia asilimia 2 ya pato lake jumla la taifa hadi kufikia 2024. Kwa sasa Ujerumani inachangia asilimia 1.2 ya pato lake la taifa kwa ajili ya bajeti ya NATO.  Kiongozi huyo wa Ujerumani aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na rais Trump kwamba ameridhishwa na ahadi iliyotolewa na rais Trump juu ya kuiunga mkono jumuiya ya NATO na juu ya kuunga mkono mchakato wa kuleta amani nchini Ukraine katika msingi wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Minsk.

Kuhusu uhamiaji na sera za Trump

USA Merkel und Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Bourg

Kwa mara nyingine viongozi hao wa mataifa makuu ya magharibi walitafautiana juu ya swala la wakimbizi. Rais Trump alimwambia kansela Merkel kwamba uhamiaji ni swala la hisani na sio haki, akiijibu kauli hiyo kansela Merkel aliutetea msimamo wake juu ya wakimbizi pia alimwambia mwenyeji wake kwamba ni vizuri zaidi kujadiliana kuliko kusengenyana. Hata hivyo kansela Merkel amekubaliana na rais Trump juu ya kusisitiza umuhimu wa kulitatua swala la uhamiaji kwa kupambana na vitisho vya itikadi kali. Bibi Merkel pia amesisitiza haja ya kuwepo mipaka imara lakini pia amesema ni muhimu kuwasaida watu katika nchi zao barani Afrika na katika Mashariki ya kati kabla hawajageuka kuwa wakimbizi.

Kabla ya kansela wa Ujerumani kuanza ziara yake nchini Marekani viongozi wa kisiasa na kibiashara wa Ujerumani walielezea wasiwasi wao juu ya sera ya rais Trump ya kuyaweka maslahi ya Marekani mbele maarufu kama "Marekani Kwanza" hata hivyo rais huyo wa Marekani alifanunua kwa waandishi wa habari kwamba yeye anaunga mkono sera ya biashara huru lakini alisisitiza kwamba anataka biashara ya haki. Kwa upande wake kansela Merkel ameitetea sera ya dunia utandawazi. Licha ya tofauti zao rais Trump amesema anataka kuwa na uhusiano wa karibu katika kufanya kazi na kansela Merkel ikiwa atachaguliwa tena. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyeongozana na ujumbe wa wafanyabiashara amemaliza ziara yake na yumo njiani kurudi nyumbani.

Mwandishi: Zainab Aziz //dw.com/p/2ZSZo

Mhariri: Iddi Ssessanga