Merkel na Pelosi wakubaliana juu ya hali ya hewa
29 Mei 2007Tayari serikali chini ya rais Bush iliarifu, kwamba mapendekezo aliyoyatoa Merkel hayaendi sambamba na malengo ya Kimarekani. Hata hivyo, Kansela Merkel hajakata tamaa. Ndio maana leo amekutana na kiongozi wa upinzani katika baraza la wawakilishi la bunge la Marekani, Bi Nancy Pelosi.
Baada ya mkutano wake na kiongozi wa upinzani huko Marekani, Nancy Pelosi, Kansela Angela Merkel alisisitiza kuwa ataendelea kudai viongozi wa nchi za G8 wayakubali masharti ya kulazimisha ili kupambana na ongezeko la joto duniani.
Bi Merkel alisema: “Tunaamini nchi za kiviwanda lazima zitoe mfano mzuri. Tunakubaliana kuwa teknolojia na uvumbuzi wa teknolojia mpya ni muhimu zaidi. Bila shaka, itabidi tuwe na mazungumzo juu ya namna tunavyoweka ghamara kwa utoaji wa gesi ya Corbondioxide na kuweka masharti ya kulazimisha. Lakini hadi hapa tulikuwa na mjadala mzuri na mrefu. Na naamini kuhusiana na suala hilo, mambo yanabadilika nchini Marekani.”
Bi Pelosi, kwa upande wake, alimshukuru Kansela Merkel kwa kuchukua jukumu kubwa katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Katika taarifa yake, Pelosi alitaka kutumwe zaidi teknolojia za kisasa ili kupunguza ongezeka la joto duniani.
Licha tu ya hajakubali wazi masharti ya kimataifa, Pelosi alikiri inabidi nchi nyingi zishirikiane kusimamisha mabadiliko ya hali ya hewa. Bi Pelosi amesema: “Namuunga mkono kabisa Kansela Merkel pale anaposema matatizo haya yanaweza kutatuliwa tu kwa ushikamano wa dunia zima, na kuwa masuluhisho yawe endelevu. Nchini mwangu kuna watu wengi ambao kama mimi wanaamini dunia hii imeumbwa na Mungu, na ni jukumu letu kuhifadhi uumbaji huu.”
Msimamo wa serikali ya Marekani ni kuwekeza katika teknolojia za kisasa zinazolinda mazingira, lakini itakataa kukubali malengo ya pamoja ya kupunguza utoaji wa gesi chafu. Tayari kabla ya mkutano wa kilele wa juma lijalo, serikali chini ya rais George Bush ililikataa pendekezo la Ujerumani ambalo linasema utoaji wa gesi zinazoharibu hewa upunguzwe hadi kufikia nusu ya kiwango cha mwaka 1990 mnamo miaka 30 ijayo.
Wiki iliyopita, Bi Merkel, mbele ya bunge la Ujerumani, alisema hana uhakika ikiwa kutafikiwa makubaliano kwenye mkutano wa G8 juu ya muda wa baada ya maafikiano ya Kyoto yatakapoisha mwaka 2012 na masharti ya kupunguza utoaji wa Carbondioxide. Katika azimio la mwisho wa mkutano ujao wa G8, serikali ya Ujerumani inataka liandikwa sharti la kwamba joto la wastani duniani lisiongezeke zaidi ya digrii mbili. Juu ya hayo, inambidi sasa Kansela Merkel afikie mwafaka na rais Bush.