Merkel na Obama waujadili mgogoro wa Ukraine mjini Washington
10 Februari 2015Mhariri wa gazeti la " Volksstime" anasema Rais wa Marekani Barack Obama na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanalo jambo la pamoja, nalo ni kwamba wote hawaliungi mkono wazo la kuipelekea silaha Ukraine.
Hata hivyo mhariri huyo anatilia maanani kwamba pana tafouti kati ya kile ambacho mtu anadhamiria kukifanya na kile ambacho mtu analazimika kukifanya.
Mhariri huyo anasema hilo ni jambo la kawaida katika siasa. Kwani Rais Obama sasa anazidi kushinikizwa na maseneta wa chama cha Republican na hata wale wa chama chake, kumtaka achukue hatua madhubuti dhidi ya Urusi nchini Ukraine.
Nchi za magharibi zimesimama pamoja juu ya Ukraine
Gazeti la "Bild" linasema ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Marekani imethibitisha nguvu ya mshikamano wa nchi za magharibi.
Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba baada ya ziara ya Kansela Merkel nchini Marekani na baada ya mazungumzo baina ya Kansela huyo ,Rais Hollande wa Ufaransa na Rais wa Urusi Wladimir Putin jambo moja sasa limethibiti kuwa wazi: rafiki wa dhati wanaweza kukaa chini na kuzungumza juu ya matatizo yao.Kansela Merkel na Rais Obama wameweza kuelewana juu ya suala la kuipa silaha Ukraine, na sasa wameupata msimamo wa pamoja juu ya suala hilo. Subira inaweza kuleta heri,
Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Reut-linger General Anzeiger" anaonya katika maoni yake kuwa ikiwa Rais Putin hatakuwa tayari kufikia mwafaka,wanasiasa wengi barani Ulaya wataliunga mkono wazo la kuipa silaha Ukraine ili iweze kujihami dhidi ya Urusi. Kwa sababu jambo moja lipo wazi kabisa ,kwamba kadri mapigano yanavyozidi kuendelea, ndivyo Ukraine itakavyohitaji kusaidiwa kwa kupewa silaha.
Jee ni nani wa kumpigia simu barani Ulaya ?
Katika maoni yake gazeti la "Westfälische Nachrichten" linarudi nyuma kidogo katika historia na kulikumbuka swali la aliekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Henry Kissinger. Kissinger aliuliza wakati huo, jee mtu akitaka kuzungumza la Ulaya ampigie simu nani?
Mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten" anaeleza kuwa sasa jibu la swali hilo limepatikana. Nalo ni Angela Merkel!. Siku nyingi Marekeni imekuwa inataka kuiona Ujerumani ikiwa na sera ya mambo ya nje thabiti na huru.Obama anaelekea kuuunga mkono msimamo wa Kansela Merkel wa kuizingatia diplomasia, na ndiyo sababu kwamba sasa yupo tayari kusubiri juu ya suala la kuipa silaha Ukraine.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Yusuf Saumu