1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Li watafuta ushirikiano zaidi wa kibiashara

Caro Robi
9 Julai 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema nchi yake na China zote zimejitolea kuheshimu makubaliano ya kibiashara yanayohusisha pande mbali mbali na sheria za biashara zinazotambulika duniani.

https://p.dw.com/p/315k0
Merkel und Ministerpräsident der Volksrepublik China Li Keqiang im Bundeskanzleramt Berlin
Picha: DW/Irfan Aftab

Viongozi hao wawili wamejadili sera za kulinda viwanda vya nchini, suala linaloathiri biashara duniani hasa kutokana na hatua za Marekani za kuziongeza kodi bidhaa kutoka China na katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa kiserikali leo mjini Berlin, ambapo makubaliano kadhaa ya ushirikiano wa kibiashara kati ya kampuni za Ujerumani na China yalitiwa saini, Merekel pia ameisifu China kwa kuyafungua masoko yake ili kuendeleza uwekezaji wa kigeni.

Kansela huyo wa Ujerumani amesema nchi zote mbili zinataka kudumishwa kwa sheria za shirika la biashara duniani WTO, na amejadili kwa kina na Li kuhusu suala la kuwa na biashara huru zaidi. Kumekuwa na wasiwasi miongoni mwa maafisa wa Umoja wa Ulaya kuwa kampuni za China zinapata urahisi kuwekeza Ulaya kuliko jinsi kampuni za Ulaya zinavyoweza kuwekeza China.

Ujerumani yatafuta ushirikiano zaidi na China

Merkel amesisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano unaoweza kutegemewa kati ya China na Ujerumani hasa wakati huu ambapo kuna ukosefu wa usalama duniani. Kwa upande wake, Li amemueleza Merkel kuwa China kwa hakika inataka kuuendeleza uhusiano utakaozinufaisha pande zote mbili.

Deutschland 5. deutsch-chinesische Regierungskonsultationen
Merkel, Li na mawaziri wa China na Ujerumani mjini BerlinPicha: Reuters/F. Bensch

Viongozi wa kibiashara wa Ujerumani wanautiazama mkutano huo kati ya nchi yao na China, nchi zote mbili zikiwa na nguvu kubwa duniani ya kuuza kwa wingi zaidi bidhaa zao nje ya nchi, kupata ishara ya wazi kisiasa itakayopinga vikwazo vinavyozidi kuongezeka vya kibiashara na pia kupata soko huru zaidi la China.

Mkutano huo kati ya Merkel na Li unakuja wakati ambapo mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani kuhusu nyongeza ya kodi za bidhaa kadha wa kadhaa ukitishia kugeuka kuwa vita vya kibiashara, vitakavyokuwa na athari kubwa duniani.

Marekani pia imeziongezea kodi bidhaa za chuma na bati za Umoja wa Ulaya, huku Rais wa Marekani Donald Trump hususan akiilenga zaidi Ujerumani hasa sekta yake ya magari. Marekani inaishutumu China kwa wizi wa kazi za ubunifu na kuathiri shughuli za kiteknolojia kutokana na sera zake za kiuchumi.

China nayo imejibu kwa kuziongezea kodi bidhaa za Marekani za kilimo, zikilenga wafuasi wa Trump walioko katika maeneo ya vijijini. Pia imeyawekea kodi ya juu magari yanayoingizwa nchini China kutoka Marekani.

Hiyo inamaanisha kuwa itaziathiri kampuni za Ujerumani kama Daimler na BMW, ambazo zina viwanda Marekani vya kuunganisha sehemu za magari yanayouziwa soko kubwa la China.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef