Merkel: Muungano wa Ujerumani haujakamilika
3 Oktoba 2018Ujerumani leo imesherehekea miaka 28 tangu kuungana tena kwa upande wa Magharibi na Mashariki, mchakato ambao Kansela Angela Merkel amesema bado haujakamilika. Viongozi wa taifa hilo wameelezea wasiwasi kuhusu migawanyiko inayoikumba jamii ya taifa hili na kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo.
Ujerumani iliunganishwa tena Oktoba 3, 1990, kufuatia mgawanyiko wa vita zaidi uliodumu kwa zaidi ya miongo minne, na chini ya mwaka mmoja tangu Ujerumani Mashariki iliokuwa inafuata misingi ya kikomunisti kufunga mpaka wake wenye ulinzi mkali.
Licha ya hatua kubwa kupigwa tangu wakati huo, tofauti za kiuchumi na nyingine zinaendelea kuwepo kati ya upande wa mgharibi, na mashariki isiyo na mafanikio makubwa.
Matamshi ya viongozi wa Ujerumani katika sherehe ya kuadhimisha muungano huu zilizofanyika leo mjini Berlin, yameakisi wasiwasi kuhusu migawiko ndani ya jamii ya Ujerumani - ambayo kwa kiasi kikubwa iko kwenye misingi ya mashariki na magharibi.
Merkel: Muungano wa Ujerumani haujakamilika
Kansela Merkel, ambaye alikulia katika Ujerumani ya Mashariki, amesema "muungano wa Ujerumani bado haujakamilika" na bado unaendelea kutoa changamoto hadi hii leo. Miaka 28 baadae, tunajua kwamba kile tunachokiita muungano wa Ujerumani ni mchakato, ni barabara ndefe, ambayo inatupasa tena na tena kusikilizana, amesema Merkel lakini akaongeza kuwa.
Kuwasili kwa idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wengine katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumesababisha mgawanyiko na malalamiko makubwa nchini Ujerumani.
Chama cha siasa kali za kizalendo cha Alternative für Deutschland - Au Chama Mbadal kwa Ujerumani - AfD, ambacho kinaungwa mkono katika maeneo mengi ya nchi, lakini chenye ngome yake katika upande wa mashariki, kilipata uwakilishi bungeni mwaka uliopita.
Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na suala tete la wahamiaji
Maandamano ya vurugu ya wafuasi wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia ya mwezi uliyopita kufuatia kuuawa kwa mwanaume wa Kijerumani na wanaodaiwa kuwa wahamiaji katika mji wa mashariki wa Chemnitz, yameongezea kwenye wasiwasi huo.
"Hatutoruhusu kugawanywa, amesema Meya wa Berlin Michael Mueller katika sherehe kuu ya siku hii iliyofanyika katika jumba la michezo la Staatsoper mjini humo, na kuongeza kuwa hili siyo suala la mashariki na magharibi.
Naye spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaeuble, ambaye alisaidia kujadili kuunganishwa tena kwa Ujerumani, amesema wanasiasa wa kizalendo wamekuwa wakiwachochea watu dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa, dhidi ya jamii za wachache na dhidi ya wale waliochaguliwa na watu, na kuongeza kuwa hakuna mwenye haki ya kusema kuwa yeye pekee ndiye anawakailisha watu.
Mhariri: Grace Patricia Kabogo