Merkel : Mazungumzo ya tabia nchi na Trump hayaridhishi
28 Mei 2017Azimio la G7 sasa litampa muda zaidi Rais huyo wa Marekani kuamuwa iwapo aiachie Marekani iendelee kubakia katika mkataba wa Paris wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambao mtangulizi wake Barack Obama aliusaini mwaka 2015.
Azimio lililotolewa na nchi za kundi hilo la mataifa saba limesema Trump aliyehudhuria mkutano wa kilele wa G7 kuhusu tabia nchi na masuala ya usalama amekiri kwamba Marekani ilikuwa bado ingali "inatathmini sera zake juu ya mabadiliko ya tabia nchi na juu ya makubaliano ya Paris na kwamba nchi hiyo haiko katika nafasi ya kujiunga na muafaka juu ya masuala hayo."
Viongozi wote sita wameahidi kujitolea kwa makubaliano hayo ya Paris.Baadae Trump aliandika kwenye mtandao wa twitter kwamba atatowa uamuzi wake wa mwisho kuhusiana na makubaliano ya Paris wiki jayo.
Mazungumzo hayaridhishi kabisa
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyaelezea mazungumzo hayo kuhusu tabia nchi kuwa "hayaridhishi kabisa" na kuongeza wamba hakuna dalili iwapo Marekani itaendelea kubakia katika makubaliano hayo la.
Merkel amesema makubaliano ya Paris ni muhimu sana na kwamba hakupaswi kuwepo mjadala wa kutafuta muafaka kwa suala hilo kwani makubaliano hayo ya Paris si tu kama makubaliano mengine " ni makubaliano muhimu ambayo yanajenga utandawazi leo hii."
Merkel amesema nchi saba tajiri zenye maendeleo makubwa ya viwanda na demokrasia zilizokuwa zikikutana katika mkutano wa kilele huko Sicily Italia zilikuwa na majadiliano ya hoja za msingi kuhusu biashara na zimekubaliana kupinga hatua za kulinda masoko.
Biashara huru
Makubaliano hayo yamekibakisha kifungu kilichoafikiwa katika mikutano iliopita kutokana na kuwepo kwa mtizamo mpya kutoka kwa Rais Donald Trump ambaye amesisitiza biashara lazima izingatie haki halikadhalika iwe huru.Merkel amesema viongozi wamekubaliana kuchukuwa hatua dhidi ya kupinga hatua za kulinda masoko.
Wakati wa kampeni za urais mwaka jana Trump aliahidi kuanzisha upya mazumgumzo hayo ya makubaliano ya kihistoria ya Paris kuhusu tabia nchi na hata kutishia kujitowa kabisa. Tokea aingie madarakani amekuwa akizirudisha nyuma taratibu za kutowa gesi zenye kuchafuwa mazingira kwa kusema kwamba taratibu hizo ni mbaya kwa kampuni za Marekani.Marekani inaendelea kubakia kuwa mtowaji mkubwa wa gesi chafu zenye kuathiri mazingira ikitanguliwa na China.
Iwapo Trump atajitowa kwenye makubaliano hayo ya Paris au la ni jambo lisilojulikana.Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Kiuchumi nchini Marekani Gary Cohn amesema mawazo ya Trump yanabadilika na kwamba amekwenda huko kujifunza na kuzidi kuwa mtu wa busara.Gary alikuwa akizungumza hayo hapo Ijumaa baada ya kuulizwa kuhusu mawazo ya rais juu ya makubaliano ya tabia nchi.Mshauri wa usalama wa taifa H.R McMaster ambaye alikuwa pembezoni mwa Cohn amesema Trump atatowa uamuzi kwa kuzingatia kile kilicho bora kwa wananchi wa Marekani.
Shirika la hisani la Uingereza la Oxfam limeutaja msimamo wa mkali wa G7 inaoaminika kushawishiwa sana na Trump kuwa ni "kashfa ."Sicily inaambatana na bahari ambapo watu 1,400 wamekufa maji mwaka huu pekee na ambako mamia kwa maelfu ya wahamiaji wamejihifadhi baada ya kukimbia vita na umaskini katika nchi zao za Kiafrika.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters/AFP/dpa
Mhariri : John Juma