Merkel kuanza ziara Marekani
26 Aprili 2018Kansela Angela Merkel anakabiliwa na mtihani wake mkubwa kufuatia mwanzo ambao haukuwa mzuri katika muhula wake mpya madarakani akiwa kama mkuu wa taifa lenye uchumi mkubwa barani Ulaya wakati atakapokutana na rais wa Marekani Donald Trump leo katika juhudi zake za kuonesha mamlaka ya kisiasa ya Ujerumani mjini Washington.
Biashara itakuwa mada muhimu ya majadiliano katika mkutano wa viongozi hao wawili, kabla ya msamaha wa ushuru wa forodha katika bidhaa za chuma na bati uliotolewa kwa Umoja wa Ulaya kumalizika muda wake hapo Mei mosi.
"Kwa mtazamo wa hivi sasa, mtu anapaswa kutarajia kwamba ushuru utaanza Mei mosi," afisa mmoja alisema, akisisitiza kwamba Ujerumani itaendelea na majadiliano kuhusiana na suala la biashara na kujaribu kufikia makubaliano mapana zaidi katika viwanda.
"Tunataka kujadili ushuru wa viwanda kwa jumla," afisa huyo amesema, akidokeza kwamba, "Kuna tofauti fulani ndani ya Umoja wa Ulaya."
Ziara ya siku moja ya Merkel inafuatia ziara ya siku tatu mjini Washington iliyofanywa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Merkel kumshawishi Trump kuhusu Iran
Macron aliitaka Marekani kutoachana na makubaliano ya kimataifa ya kinyuklia na Iran wakati mabalozi wa mataifa ya magharibi wamesema Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wanakaribia kufikia makubaliano ambayo yanataka kumshawishi Trump kuokoa mkataba huo.
Trump ameueleza mkataba huo wa mwaka 2015, ambao Iran imekubali kuzuwia shughuli zake za kinyuklia ili kuweza kupata kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, kuwa ni makubaliano mabaya kabisa kuwahi kujadiliwa na ametishia kuyavunja kwa kurejesha vikwazo vya Marekani mwezi ujao, iwapo washirika wake wa Ulaya hawatakubali kuutengeneza upya kurekebisha mapungufu yake.
Pamoja na hayo ziara ya Merkel nchini Marekani inakuja huku kukiwa na hatari kwa kansela huyo mwenye umri wa miaka 63, ambaye amekuwa na mwanzo mbaya katika uhusiano wake na Trump.
Hii imekuja baada ya Trump kuushambulia vikali msimamo wa kiliberali wa Merkel kuhusu wakimbizi katika kampeni yake ya urais mwaka 2016, akiueleza kuwa ni maafa, na kutaka serikali ya Ujerumani ipunguze nakisi yake kubwa ya biashara na Marekani pamoja na kuongeza mchango wake katika jukumu la kuiendesha jumuiya ya NATO.
Ziara muhimu kwa Merkel
Merkel ambaye huchukua tahadhari mno ameshindwa kutengeneza uhusiano wa binafsi na Trump na hali ya ziara yake katika Ikulu ya Marekani ya White House bila shaka itatofautiana kwa kiasi kikubwa na ziara ya Macron iliyokuwa na mvuto mkubwa wa mapenzi kwa viongozi wote wawili.
"Kansela anafurahia ziara hii kwasababu anaamini katika uhusiano kati ya Marekani na Ulaya," mmoja kati ya maafisa alisema. "Ni muhimu kujenga uhusiano huu."
Mtaalamu wa uchumi katika benki ya ING nchini Ujerumani Carsten Brzeski, amesema kwamba "ziara ya Merkel itawakilisha fursa ya kwanza kwa kansela huyo kuona iwapo Marekani bado inamuona kuwa ni kiongozi mkuu wa Ulaya."
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre
Mhariri: Josephat Charo