Merkel, Hollande kukutana
23 Agosti 2012Viongozi hao wa mataifa yenye uchumi mkubwa katika kanda ya sarafu ya Euro wanajaribu kuonyesha umoja kwenye mzozo huo, ikiwemo namna ya kulitatua tatizo la Ugiriki.
Wanatarajiwa kumwambia Waziri Mkuu wa Ugiriki, Antonis Samaras, kwamba hawezi kufanya jambo lolote kinyume na makubaliano ya mpango wa kubana matumizi ili apate msaada wa kuikokoa nchi yake.
Merkel na Hollande watakutana jioni ambapo watakubaliana kwa kauli moja juu ya juhudi za Samaras za kutaka kupewa muda zaidi kwa nchi yake itimize makubaliano ya kubana matumizi. Kwa mujibu wa ripoti kutoka Ugiriki, Samaras anataka nyongeza ya muda wa miaka miwili.
Viongozi wa ngazi za juu hapa Ujerumani wameshasema kuna fursa ndogo sana kwa Samaras kufanikiwa katika mpango wake, huku Kansela Merkel mwenyewe akaongezea msumari na kuweka bayana kuwa hilo haliwezekani.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anajiuliza ni namna gani watashirikiana na Ugiriki
Msimamo wa Kansela Merkel
Wakati wa safari yake nchini Moldovo hapo jana, Kansela Merkel aliwaambia waandishi wa habari kwamba anakwenda kwenye mkutano na Hollande akiwa anajua wazi kichwani mwake kwamba ni lazima watimize malengo yao kwa kila moja kutimiza wajibu wake.
Kansela Merkel huenda akampa funzo Rais Hollande kuwa hata yeye anaweza kuonyesha mfano kwa kutekeleza sera ya kubana matumizi kwenye bajeti ya Ufaransa ya mwaka 2013 ambayo itawasilishwa mwezi ujao wa Septemba.
Samaras atakutana na Kansela Merkel kesho na kisha atakutana na Hollande keshokutwa. Merkel ameshasema kuwa hakuna suluhu itakayopatikana katika mkutano wake na Samaras. Maamuzi yote yatasubiri hadi hapo wataalamu wa masuala ya uchumi wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la kimataifa, IMF, watakapotoa mapendekezo yao.
Ukimya wa Hollande
Kwa upande wake, Hollande ambaye ndio kwanza amerejea kutoka mapumziko ya msimu wa kiangazi barani Ulaya, anaonekana na yuko kimya sana kuhusu msimamo wake kwa Ugiriki tofauti na mwenzie.
Wachambuzi nchini Ufaransa wanasema kuwa nchi hiyo haiwezi kumudu kuendelea kuipa fedha Ugiriki kwa kuwa yenyewe inaangalia namna ya kujiinua kiuchumi baada ya kudorora kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka.
Shinikizo linazidi nchini Ujerumani la kutaka Benki Kuu ya Ulaya iingilie kati katika masoko ya dhamana za mikopo kwenye serikali mbalimbali, hatua ambayo itapunguza kiwango kikubwa cha kukopa kwa Uhispania na Italia.
Ujerumani inapinga kitendo cha kuitumia Benki Kuu ya Ulaya kutatua mizozo ya uchumi ya nchi zenye hali mbaya, wakati Hollande alichaguliwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa ahadi yake ya kuwa Ufaransa itashirikiana na kanda ya sarafu ya Euro kuubeba mzigo wa madeni.
Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman