Merkel : Hatua za kijeshi haziwezi kutatuwa mzozo wa Syria
4 Oktoba 2015Akizungumza na kituo cha radio cha taifa Deutchlandfunk katika mahojiano yaliyorushwa Jumapili (04.10.2010) Merkel amesema mchakato wa kisiasa unahitajika kukomesha vita vya Syria juu ya kwamba kuingilia kati kijeshi pia ni muhimu.
Amekaririwa akisema "kuhusiana na suala la Syria tutahitaji hatua za kijeshi lakini hatua za kijeshi pekee haziwezi kuutatuwa mzozo huo,tunahitaji mchakato wa kisiasa ambao hadi sasa umekuwa vigumu kutekelezeka."
Katika kauli ya moja kwa moja ambayo hakuwahi kuitumia kabla kongozi huyo wa Ujerumani amesisitiza kamba utawala wa sasa wa Rais Bashar Assad lazima ushirikishwe katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Syria uliodumu kwa zaidi ya miaka minne.
Mataifa yamekuwa yakitafautiana juu ya iwapo Assad anapaswa kuwa na dhima yoyote ile kwa mustakbali wa Syria.
Uwakilishi wa serikali ya Syria
Amesema kufanikisha mchakato huo wa mazungumzo kunahitajika kuwepo kwa wawakilishi wa upinzani wa Syria halikadhalika wale wa serikali ilioko Damascus pamoja na wahusika wengine.
Merkel amekumbusha kwamba tayari wawakilishi wa Assad wamekuwa wakishiriki katika duru mbali mbali za mazungumzo yaliokuwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Amesema "hii haimaanishi kwamba hawaoni juu ya ukatili unaotendeka nchini Syria ikiwa ni pamoja na kile alichokifanya Assad na anachoendelea kufanya kwa kutumia mabomu ya mapipa dhidi ya wananchi wake mwenyewe.
Marekani na Urusi zina dhima
Merkel amesema Marekani na Urusi zinaweza kutimiza "dhima muhimu" na kwamba amezungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi kuhusu mzozo huo wa Syria wakati wa mazungumzo yao mjini Paris wiki iliopita pembezoni mwa mkutano kuhusu mzozo wa Ukraine.
Pia amezitaja Saudi Arabia, Iran halikadhalika Ujerumani, Ufaransana Uingereza kama wahusika wengine wanaopaswa kushiriki katika mazungumzo hayo.Amesema "Sisi Ulaya pia tuna wajibu."
Marekani na Ufaransa zimefanya mashambulizi ya anga nchini Syria na Urusi imefanya mashambulizi yake ya kwanza ya anga nchini Syria kwa kile ilichosema dhidi ya wapiganaji wa jihadi wa kundi la Dola la Kiislamu.
Lakini Ujerumani mara kwa mara imekuwa ikifuta uwezekano wa kujihusisha kijeshi katika mzozo huo.
Sheria za hifadhi kutodhoofishwa
Akizungumzia mzozo wa wakimbizi barani Ulaya ambao kwa kiasi fulani umesababishwa mzozo huo wa Syria Merkel pia ameiambia radio hiyo ya taifa kwamba Ujerumani haitodhoofisha sheria zake za kuwapa hifadhi watu wenye mahitaji hayo ambazo zinataka wale wote wenye madai halali ya kupatiwa hifadhi wapokelewe.
Hata hivyo amesisitiza mchakato wa kuomba hifadhi itabidi uimarishwe na kwamba wahamiaji wasiostahiki kupatiwa hifadhi watatakiwa wondoke Ujerumani.
Merkel amekua akipongezwa na kulaumiwa kwa namna alivyoushughulikia mzozo huo wa wakimbizi.Ujerumani hivi sasa inakabiliwa na wimbi kubwa la mmiminiko wa wahamiaji wengi wao wakiwa wakimbizi wanaokimbia kutoka nchi kama vile Syria na Afghanistan. Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni moja yumkini wakatafuta hifadhi nchini Ujerumani kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Kauli hiyo ya Merkel inakuja kufuatia miito kutoka kwa chama ndugu cha CSU cha Bavaria chenye kuunda muungano wa kihafidhina kwa kushirikiana na cha Merkel cha CDU kudhoofisha kipengele hicho cha sheria cha kuwapokea watafuta hifadhi kutokana na nchi kuelemewa na mzigo wa idadi kubwa ya wahamiaji wanaoendelea kuwasili.
Uzio sio suluhisho
Merkel amekataa pendekezo la kuitaka Ujerumani iweke uzio kwenye mipaka yake kwa kusema kwamba halifai.Amesema "Sifikirii uzio unaweza kusaidia.Tumeona hilo nchini Hungary."
Hungary hivi karibuni imeweka uzio wa senyen'ge kwenye mipaka yake na nchi za Balkan katika jaribio la kuzuwiya wahamiaji wasiingie Ulaya hatua ambayo imepelekea kulaaniwa na nchi wanachama wenzake wa Umoja wa Ulaya.
Merkel pia ameutetea uamuzi wake wa kuifunguwa mipaka ya Ujerumani kwa wakimbizi ambao hususan umekosolewa na kiongozi wa chama CSU Horst Seehofer kwa kusema kwamba angeliurudia tena uamuzi huo.
Juu ya kwamba aliupinga uamuzi huo wa Merkel alioutowa mwezi wa Septemba Seehofer hajajiunga na miito kutoka ndani ya chama chake mwenyewe kutaka kufanyiwa marekebisho kwa sheria za kuomba hifadhi.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri : Iddi Sessanga