Merkel asema hana majuto kuhusu utawala wake
26 Novemba 2024Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel ameitetea miaka 16 ya utawala wake katika kitabu chake kwa jina Freedom yaani Uhuru, kilichotolewa katika lugha 30 leo Jumanne.
Tangu alipoondoka madarakani Merkel amekuwa akituhumiwa kwa kuwa na msimamo mwepesi kuhusu Urusi, akiiwacha Ujerumani ikiwa tegemezi kwa gesi ya bei nafuu ya Urusi na kuchochea machafuko na kuimarika kwa siasa za kizalendo za mrengo mkali wa kulia kwa sera yake ya uhamiaji ya milango wazi.
Kitabu chake kimetolewa huku vita nchini Ukraine na Mashariki ya Kati vikiendelea, na Donald Trump akitarajiwa kuapishwa Januari mwakani kurejea ikulu na Ujerumani ikikabiliwa na uchaguzi wa mapema baada ya muungano unaotawala kusambaratika mwezi huu.
Merkel, mwenye umri wa miaka 70, amesema hana majuto na anakataa lawama kwa machafuko yoyote ya sasa katika kitabu chake cha kurasa 763, alichokiandika kwa ushirikiano na mshauri wake wa muda mrefu Beate Baumann.