1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel hafuti uwezekano wa serikali ya muungano mkuu

17 Agosti 2013

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hafuti uwezekano wa kuongoza serikali ya muungano mkuu baada ya uchaguzi kutokana na wasi wasi iwapo washirika wake wa FDP wanaweza kushinda viti vya kutosha kuweza kuingia bungeni.

https://p.dw.com/p/19RYt
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters

Akizungumza katika mahojiano yaliochapishwa katika toleo la Jumamosi(17.08.2013) la gazeti la Frankfurter Allgemeine, Kansela Angela Merkel amesema anategemea uchaguzi huo kuwa wa mchuano mkali na kwamba kufuta uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu kati ya chama chake cha Christian Demokratik (CDU) na chama cha Social Demokratik (SPD) litakuwa ni jambo lisilowezekana kabisa.Hata hivyo amesema kwamba hakuna anayechukuwa hatua kuelekea kuundwa kwa serikali ya aina hiyo na kwamba itakuwa ni bora kwa Ujerumani iwapo chama cha CDU kitaweza kuendelea kuongoza na washirika wake wadogo wa hivi sasa chama cha kiliberali cha Free Demokratik (FDP).

Merkel tayari aliwahi kuongoza mara moja serikali ya muungano mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ambapo mpinzani wake mgombea wa ukansela kutoka chama cha SPD Peer Steinbrück alikuwa waziri wa fedha ambaye amefuta uwezekano wa kukiingiza chama chake katika serikali nyengine ya muungano mkuu. Katika toleo la Jumamosi la gazeti la Hamburger Morgenpost amesema wamepitia jambo hilo kati ya mwaka wa 2005 na 2009. Ameongeza kusema kwamba kusema kweli wanachama na wabunge wengi wa chama hicho hawataki kurudia jambo hilo.

Steinbrück pia amedokeza kwamba kwa kuzingatia kipindi cha muda mrefu kujiunga katika serikali ya muungano mkuu yumkini kukawa hakuna maslahi mazuri ya kisiasa kwa chama chake.Amesema juu ya kwamba chama cha SPD kilikuwa mshirika wa kuaminika na mwenye wasifu madhubuti umashuhuri wake ulishuka hadi kufikia asilimia 29 hapo mwala 2009.

Kibaruwa kigumu kumbwaga Merkel

Mpinzani huyo wa Merkel bado ana uwezo wa kurudi kwenye umashuhuri lakini bado haionekani kama Steinbrück atakuwa kansela mpya wa Ujerumani.Kijujuu anaonekana kama ni mtu anayefaa aliekuja kwa wakati muafaka:ni mtaalamu wa fedha na ana maarifa ya ndani juu ya mzigo unaoukabili bajeti ya taifa.Atakuwa na kibaruwa kigumu kuweza kumpinduwa bosi wake huyo wa zamani. Kuna sababu kadhaa za kun'gara kwa Merkel.Amefikia kipeo cha maisha yake ya kisiasa.Hana mpinzani ndani ya chama chake na anadhibiti mzozo wa hivi sasa wa sarafu ya euro na madeni barani Ulaya katika makao makuu ya umoja huo mjini Brussels. Wajerumani wengi wanamheshimu na kumhusudu kwa jambo hilo. Kwa hiyo kuna nafasi ndogo ya kuweza kushambuliwa na chama cha SPD na Steinbrück.

Mgombea wa Ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück.
Mgombea wa Ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück.Picha: picture-alliance/dpa

Serikali ya muungano mkuu suluhisho la dharura

Kwa jinsi mambo yanavyoonekana hivi sasa kikwazo pekee cha Merkel kitakuwa chama cha FDP washirika wa sasa katika serikali yake ya mseto.Hali baina ya vyama hivyo haikuwa nzuri katika siku za hivi karibuni. Kutokana na kuanza kupamba moto kwa kampeni za uchaguzi wanasiasa wa kiliberali mara kwa mara wamekuwa mstari wa mbele kukishutumu chama cha Merkel.Muungano wa chama CDU na CSU unataka kuongeza mafao ya mtoto, kuongeza malipo ya uzeeni na kuweka udhibiti wa kodi kwa wapangaji mambo ambayo chama cha FDP inaona yanakwenda kinyume na nidhamu ya bajeti inayodhibiti ongezeko la madeni ya serikali.

Mwenyekiti wa FDP Philipp Roesler (kulia) na mkuu wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni Rainer Bruederle.
Mwenyekiti wa FDP Philipp Roesler (kulia) na mkuu wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni Rainer Bruederle.Picha: Reuters

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha televisheni ya taifa cha ARD wiki hii umeonyesha kwamba chama cha CDU na FDP kwa pamoja vinaongoza kwa asilimia 47 ikilinganishwa na asilimia 37 ya Chama cha SPD na inaowapendelea kuwa washirika wao katika serikali ya mseto chama cha Kijani. Hata hivyo chama cha FDP kinaungwa mkono kwa asilimia tano tu ambacho ni kiwango kinachohitajika kuweza kuwa na wabunge bungeni. Iwapo kitashindwa kuvuka kiwango hicho au iwapo vyama hivyo viwili kwa pamoja vitashindwa kuwa na wingi wa kutosha wa viti bungeni na iwapo chama cha SPD na Kijani havitakuwa na viti vya kutosha kwa pamoja, Kansela Angela Merkel atalazimika kutafuta mshirika mwengine wa kuunda naye serikali ya mseto.

Kwa hiyo suluhisho pekee litakalobakia ni kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu kati ya ushirikiano wa CDU na CSU kwa upande mmoja na kwa upande wa pili chama cha SPD.

Uchaguzi mkuu wa Ujerumani unafanyika tarehe 22 mwezi wa Septemba.

Mwandishi : Mohamed Dahman/pfd/tj/dpa/AFP

Mhariri: Ssessanga, Iddi