Merkel ataka mazungumzo na Urusi yaendelee
16 Oktoba 2014Akihutubia bunge mapema leo (16 Oktoba), Kansela Merkel amesema licha ya umuhimu wa vikwazo hivyo, bado havishindi haja ya kufanyika kwa majadiliano kati ya mataifa ya Magharibi na Urusi. "Kuingilia mamlaka ya Ukraine na kuvunjwa kwa haki za majirani zetu hakukubaliki, ndiyo maana vikwazo ni hatua muhimu kwenye kuutatua mgogoro huo, lakini havitoshi, ndio maana tunasaka majadiliano na Urusi ili kuweza kupata suluhisho madhubuti zaidi," alisema.
Merkel atakutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi kandoni mwa mkutano huo, na awali alisema wangelizungumzia kwa uwazi juu ya mzozo huo wa Ukraine. Tangu mzozo wa Ukraine uanze, viongozi hao wawili wamekuwa wakizungumza mara kwa mara.
Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, amesema Putin na mwenzake wa Ukraine, Petro Poroshenko, watakutana leo katika mazungumzo ambayo yatahudhuriwa pia na Kansela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Urusi yaitaka Ulaya kuwa na hekima
Putin na Poroshenko walikutana uso kwa macho kwa mara ya mwisho mwezi Agosti nchini Belarus, ambapo ingawa walishindwa kukubaliana juu ya mpango wa amani nchini Ukraine, baadaye walifikia makubaliano mwanzoni wa Septemba. Tangu hapo, wawili hao wamekuwa wakizungumza kwa njia ya simu.
Suala la mzozo wa gesi kutoka Urusi kwenda Ukraine linatazamiwa kujadiliwa, baada ya Urusi kuikatia gesi Ukraine, ikidai malipo makubwa zaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema hapo Jumanne kwamba Putin atatumia mkutano huo wa Ulaya na Asia kuelezea sera za Urusi kuelekea Ukraine. "Natarajia mazungumzo haya yatawafanya wenzetu wa Ulaya kuwa na hekima kwenye suala hili." Alisema Lavrov.
Tangu Urusi kuichukua Rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwezi Machi mwaka huu, mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiishutumu kwa kuchochea machafuko nchini Ukraine. Marekani na Umoja wa Ulaya wameiwekea vikwazo Urusi, nayo imeanza kuchukua hatua kadhaa za kujilinda, ikiwemo kusaka washirika wengine wa kiuchumi, wakiwamo wa barani Asia.
Jumatatu iliyopita, Urusi ilisaini mikataba kadhaa ya nishati na fedha na China, wakati wa ziara iliyofanywa na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang mjini Moscow, ambaye pia anahudhuria mkutano huu wa 10 wa kilele kati ya Ulaya na Asia, mjini Milan hivi leo.
Mwandishi:Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri:Josephat Charo