1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atahitaji umakini ziara ya Uingereza

Christina Ruta27 Februari 2014

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anafanya ziara nchini Uingereza Alhamisi hii, ambako atapewa heshima ya kuyahutubia mabaraza mawili ya bunge la nchi hiyo, kabla ya kupata kikombe cha chai na Malkia Elizabeth baadaye.

https://p.dw.com/p/1BGIG
G 8 Treffen in Nordirland Cameron Merkel
Picha: Reuters

Hii ni katika kutambua hadhi yake kama mwanasiasa mwenye nguvu zaidi barani Ulaya. Lakini wachambuzi wanasema Merkel itambidi kuepusha kufanya mambo kuwa magumu zaidi kwa waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye anahitaji kujiweka mbali kidogo na Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu David Cameron atakuwa makini kumuweka Merkel upande wake wakati, viongozi hao wawili wakijadili sera ya Umoja wa Ulaya. Cameron anakabiliwa na shinikizo kutimiza ahadi aliyoitoa kwa wapiga kura wa Uingereza, ya kushinikiza mageuzi katika Umoja wa Ulaya. Amesema anataka kuwapa Waingereza kura ya maoni kuhusu uanachama wa Umoja wa Ulaya ifikapo mwaka 2017.

Cameron anajaribu kuwarudisha wapiga kura wahafidhina kutoka chama cha UKIP.
Cameron anajaribu kuwarudisha wapiga kura wahafidhina kutoka chama cha UKIPPicha: Getty Images

Akikabiliwa na uchaguzi mwakani, Cameron anajaribu kuelewa kuongezeka kwa ukosefu wa imani kwa Umoja wa Ulaya miongoni mwa umma wa Waingereza. Pia anakabiliwa na kuongezeka kwa umaarufu wa chama Huru cha Uingerza UKIP, ambacho kinaupinga Umoja wa Ulaya. Moja ya mabadiliko ya sera anayoshinikiza Cameron ni kudhibiti haki ya wahamiaji kutoka mataifa wanachama maskini zaidi wanaokwenda katika mataifa tajiri kama Uingereza kutumia fursa ya mfumo wake wa ustawi.

Wasio na imani na Umoja wa Ulaya
Wengi ndani ya chama chake cha Conservative wanaunga mkono wito wa waziri mkuu huyo wa kufanya mageuzi katika Umoja wa Ulaya. Jon Redwood, mbunge ambaye anadhani Uingereza haipaswi kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, alisema kuelekea ziara ya Merkel, kuwa wapiga kura wa Uingereza wanataka mageuzi katika nyanja mbalimbali - zikiwemo ustawi wa jamii, udhibiti bora wa mipaka yao, nishati nafuu, ulinzi bora dhidi ya mafuriko, uingiliaji mdogo katika makampuni madogo na biashara, na kuongeza kuwa katika nyanja hizo zote, Uingereza inazuwia na Umoja wa Ulaya.

Redwood alisema katika barua ya wazi kwa Kansela Merkel kwamba Uingereza iko tayari kuiunga mkono Ujerumani katika hatua zozote za maana kutatua matatizo ya nishati, mipaka ya wazi na mageuzi ya mifumo ya ustawi, lakini wakati huo huo, wapiga kura wa Uingereza wanataka kuwa na uhusiano mpya na Umoja wa Ulaya. Alisema kama wanachama wasiyotumia sarafu ya euro, wao wanataka kuelekea upande mwingine, na wanahitaji kulinda maslahi yao kama taifa huru linalofanya biashara.

Waziri mkuu David Cameron.
Waziri mkuu David Cameron.Picha: Reuters

Tayari Merkel ameashiria kuwa anaweza kuwa tayari kujaribu kumsaidia Cameron kwa kushinikiza mabadiliko katika sera ya uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika Umoja wa Ulaya, ili kudhibiti kile kinachoitwa "utalii wa manufaa" kati ya mataifa wanachama. Lakini wakati wa ziara yake, ana uwezekano mkubwa wa kumkumbusha kuwa yapo maswala yanayohitaji kushughulikiwa haraka kama vile mgogoro unaoendelea nchini Ukraine, na pia suala la uchumi wa kanda inayotumia sarafu ya euro.

Almut Moeller, kutoka baraza la masuala ya kigeni la Ujerumani, aliiambia DW kuwa changamoto ya ndani kwa mustakabali wa serikali ya Cameron imegeuka kuwa suala la jumuiya nzima ya Umoja ya Ulaya, na hilo linamleta Merkel katika mchezo. Kwa Angela Merkel, alisema swala ni kiasi gani kwenye ajenda yake kimetekwa na yanayoendelea nchini Uingereza, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Ujerumani kuendelea kuitibu kanda ya euro. Anahitimisha kuwa kuna maslahi madogo kwa Ujerumani kumsaidia David Cameron kuwaridhisha wanasiasa wake wasioupenda Umoja wa Ulaya.

Diplomasia inahitajika
Lakini Moeller anaamini Kansela Merkel atahitaji kutumia diplomasia ya juu mjini London, bila kusahau ajenda ya ndani ya kisiasa. Anasema jinsi atakavyopangilia ujumbe wake katika bunge itakuwa muhimu, kwa kuwa itambidi kwa namna fulani kujibu na kuakisi mjadala nchini Uingereza. Merkel itambidi pia kutafuta ukanda sawa kati yake na Cameron wakati wa mazungumzo ya Alhamisi. Moeller anasema atatafuta maeneo yenye maslahi sawa kwa wote, kwa mfano, ni namna gani watahakikisha kuwa soko la pamoja linafanya kazi.

Kansela Merkel atapata kikombe cha chai na Malkia Elizabeth wa pili.
Kansela Merkel atapata kikombe cha chai na Malkia Elizabeth wa pili.Picha: Getty Images

Lakini mjadala unaendelea nchini Uingereza, kuhusu nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Hili ni jambo ambalo Ujerumani italipinga, kutokana na umuhimu wa Uingereza, anasema Moeller, na kuongeza kuwa ikiwa Uingereza ambayo ndiyo ya tatu kwa ukubwa itaondoka katika Umoja wa Ulaya, hilo litamaanisha kuufanyia marekebisho ya jumla umoja huo, ambapo mamlaka itahama si kwa manufaa ya Ujerumani.

Siku ya Alhamisi, inaonekana kwamba viongozi hao wawili watakubaliana kutokubaliana juu ya baadhi ya mambo ya sera ya Umoja wa Ulaya. Lakini changamoto za ndani kwa waziri mkuu wa Uingereza zinabaki, na ikiwa atachaguliwa tena mwaka 2015, huenda akatimiza ahadi yake ya kura ya maoni juu ya mustakabali wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Mjadala juu ya jukumu la Uingereza katika Umoja wa Ulaya huenda ukaendelea kwa muda mrefu hata baada ya ziara ya Merkel.

Mwandishi: Logan Kitty
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo