1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asisitiza uhamiaji utapatiwa ufumbuzi na Ulaya

Caro Robi
16 Juni 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza kuwa suala la uhamiaji ni changamoto inayoikumba nchi za Umoja wa Ulaya na hivyo inahitaji suluhisho la pamoja kutoka nchi hizo za Ulaya.

https://p.dw.com/p/2zgJc
Deutschland 70 Jahre Soziale Marktwirtschaft Angela Merkel
Picha: Reuters/M. Tantussi

Kauli yake inakuja huku kukiwa na mivutano ndani ya serikali yake kuhusu suala hilo tete la uhamiaji, linalotishia kusababisha migawanyiko mikubwa katika vyama vya kihafidhina kinachoongozwa na Merkel cha Christian Democratic Union CDU na kile cha waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer Christian Social Union CSU.

Katika ujumbe wa video anaotoa kila wiki, Merkel amesema uhamiaji ni mojawapo ya changamoto nne watakazozijadili na viongozi wa Ufaransa, atakapokutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Jumanne ijayo pamoja na mawaziri wa serikali zote mbili.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni sera za kigeni, ulinzi na mustakabali wa kanda inayotumia sarafu ya euro.

Uhamiaji watikisa serikali ya Merkel

Migawanyiko kuhusu uhamiaji inaendelea kushuhudiwa kati ya viongozi wa serikali ya muungano nchini Ujerumani. Seehofer amemfuta kazi kiongozi wa Ofisi ya Uhamiaji na Wakimbizi baada ya kugunduliwa uvunjaji wa kanuni za kisheria na mambo ya ndani.

Deutschland 2012 | 25. Parteitag der CDU | Horst Seehofer & Angela Merkel
Waziri wa mambo ya ndani Ujerumani Horst Seehofer na Kansela Angela MerkelPicha: Imago/J. Sielski

Maamuzi ya Seehofer yanalenga kuuimarisha msimamo wa serikali kuhusu uhamiaji, kwa kuweka mpango wa kuwakatalia wale ambao hawana nyaraka rasmi na watu wanaotaka kuingia tena nchini baada ya kufukuzwa.

Waziri huyo wa mambo ya ndani, kutoka chama cha CSU cha Bavaria ambacho ni ndugu na chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU, pia amesema wakimbizi ambao tayari walisajiliwa katika nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya wanapaswa kukataliwa.

Merkel ameelezea upinzani kuhusiana na hatua kama hizo, akihofia kuwa zinaweza kuongeza mzigo wa wakimbizi kwa nchi nyingine na kuhujumu mshikamano wa Umoja wa Ulaya. Andrea Nahles, Mwenyekiti wa chama cha SPD ambacho ni mshirika katika serikali ya muungano anakilaumu chama cha CSU.

Siku ya Ijumaa, Seehofer alisema katika mahojiano kuwa Merkel alisababisha mpasuko ndani ya Ulaya, kwa kuwaruhusu mamia kwa maelfu ya wakimbizi kuingia Ujerumani mwaka wa 2015.

Suala hilo la uhamiaji linaitikisa serikali ya muungano ya Ujerumani ambayo imekuwa madarakani kwa miezi mitatu tu.

Kubadilisha sera ya Merkel ya mwaka 2015 ya kuruhusu maelfu ya wahamiaji kuingia Ujerumani, itakuwa pigo kubwa kwa kansela huyo ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 12 na itahujumu mfumo wa Schengen wa mipaka ya wazi kati ya wananchi wa Umoja wa Ulaya, isipokuwa Uingereza.

Je, Ulaya yashuhudia mzozo mwingine wa wahamiaji?

Suala hilo la uhamiaji lililotawala siasa za Umoja wa Ulaya kuanzia mwaka 2015, limerejea tena kwa kishindo katika siku za hivi karibuni. Serikali mpya ya Italia imekataa kuwapokea mamia ya wahamiaji na kuwaacha kukwama baharini.

Italien Flüchtlinge auf dem Schiff Aquarius
Meli iliyowabeba wahamiaji katika Bahari ya MediteraniaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Cavalli

Waziri wa usalama wa ndani mwenye msimamo mkali wa Italia ambaye pia ni makamu waziri mkuu, Matteo Salvini ameahidi kuzizuia meli mbili za mashirika yasiyo ya kiserikali zinazowabeba wahamiaji kutia nanga katika bandari ya nchi hiyo.

Salvini ameiwekea marufuku meli ya shirika la Ujerumani lisilo la kiserikali la Sea Eye and Mission Lifeline. Waziri huyo amesema Italia haitaki kuendeleza tatizo la uhamiaji kwa hiyo wanaofanya hivyo watafute bandari za kutia nanga.

Siku sita zilizopita Italia ilikataa meli ya Aquarius kutia nanga katika bandari yake. Meli hiyo inamilikiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Ufaransa Ujerumani na Italia. Meli hiyo hatimaye ilikubaliwa kutia nanga Uhispania baada ya kukataliwa na Malta pia.

Merkel anataka angalau wiki mbili kujaribu kufikia makubaliano ya nchi mbili na washirika wake kama Italia na Ugiriki kuhusu wahamiaji na kupiga hatua kuhusu suala hilo katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika kati ya tarehe 28 na 29 mwezi huu.

Sera ya Merkel ya kuwapokea wakimbizi ilipelekea wakimbizi na wahamiaji zaidi ya milioni 1.6 kuingia Ujerumani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na sera hiyo imelaumiwa kwa kuongezeka kwa umaarufu wa chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto cha Alternative für Deutschland AfD.

Mwandishi: Caro Robi/ap/Reuters

Mhariri: Jacob Safari