Merkel asisitiza mshikamano Umoja wa Ulaya
20 Machi 2018Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Poland wamezungumzia masuala mbali mbali ya kikanda ikiwemo hatua ya Umoja wa Ulaya katika kujibu kitendo cha kulishwa sumu mwezi huu huko Uingereza aliyekuwa jasusi wa Urusi pamoja na binti yake. Viongozi hao wamechukua msimamo wa pamoja kwa kutaka Umoja huo uchukue hatua kali kuhusu kisa hicho.
Merkel na Waziri Mkuu Mateusz Morawiecki wamefanya mazungumzo mjini Warsaw na kugusia masuala mbali mbali ya ushirikiano wa kikanda katika Umoja wa Ulaya, ambapo Kansela Merkel alisema anafuatilia mazungumzo ya kujaribu kuiona Poland inaepuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya kuhusiana na mageuzi katika mfumo wake wa mahakama ambayo yalitiwa msukumo na serikali ya kihafidhina nchini humo.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu Morawiecki amesema kwamba makubaliano ya kuutatua mvutano juu ya mfumo mpya wa sheria za mahakama nchini Poland ni suala linalohitaji maelewano ya pande zote. Tayari Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ilishasema mwezi Desemba mwaka jana kwamba Poland iko hatarini kukiuka sheria za Umoja wa Ulaya na kwamba inamulikwa.
Katika ziara hiyo fupi ya Merkel nchini Poland, yeye pamoja na kiongozi mwenzake Morawiecki walisisitiza juu ya Ulaya kuwa na ushirikiano thabiti. Na kutokana na msimamo huo, suala la mvutano kati ya Uingereza na Urusi kuhusu kitendo cha kushambuliwa kwa kemikali za sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi katika ardhi ya Uingereza, viongozi hao wamezungumzia haja ya Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali. Waziri mkuu Mateusz Morawiecki amesema,
"Tunaunga mkono hatua kali ichukuliwe na Umoja wa Ulaya kwa ujumla. Shambulio lilifanyika katika nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya na katika ardhi ya nchi mwanachama wa Jumuiya ya NATO, na tunaamini kwamba hatua ya pamoja inahitajika ili mtumiaji mabavu Urusi atambue kwamba hawezi kuendeleza sera hiyo.''
Kwa upande wake Kansela Merkel amesisitiza kuwa kwa hali ilivyo ulimwenguni, wanafahamu kwamba sauti ya Umoja wa Ulaya itakuwa na nguvu ikiwa tu Umoja huo utaendelea kuwa na mshikamano imara. Kadhalika kiongozi huyo wa Ujerumani amezungumzia kitisho cha Marekani katika suala la biashara na Umoja wa Ulaya akisema:
"Kulikuweko pia na mtazamo thabiti kuelekea kitisho cha sheria mpya za viwango vya kodi na hatua za kulinda viwanda dhidi ya ushindani wa kibiashara. Waziri wa uchumi wa Ujerumani yuko Marekani leo, na tume ya Umoja wa Ulaya itazungumzia kuhusu suala hili. Tutafanya kila tunaloweza kupata suluhu lakini nchi zote zimejitolea katika biashara huru na tunaamini kwamba kila mmoja atafaidika kutokana na hilo na hatua ya kulinda viwanda dhidi ya ushindani wa nje haitotufikisha popote."
Ziara ya Merkel nchini Poland imekuja siku chache baada ya kuingia rasmi madarakani katika muhula wake wa nne.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpae/afpe
Mhariri:Mohammed Khelef