Merkel asifiwa kwa kukutana na Dalai Lama
24 Septemba 2007Katika kuonesha kutoridhishwa kwake na hatua hiyo ya Kansela Merkel, China ilijiondoa katika ushiriki wake kwenye mkutano wa masuala ya sheria kati ya nchi mbili hizo mjini Munich. Vilevile wizara ya nje ya China ilimuita balozi wa Ujerumani mjini Beijing kulalamika ya juu ya hatua ya Ujerumani kuingilia mambo ya ndani ya China. Wahiri wa magazeti ya Ujerumani wanamuunga mkono Kansela Merkel. Tukianza na gazeti la “Augsburger Allgemeine”, mhariri wake anamsifu Angela Merkel kwa kufanya mazungumzo haya na Dalai Lama na anaendelea:
“Haitawezekana kuwa kiongozi wa serikali ya Ujerumani anaiomba China kutoa ruhusa kwa mazungumzo anayotaka kuyafanya. Hasa ikiwa ni mazungumzo na kiongozi wa kidini anayetekeleza sera za amani. Huenda China kama kuonyesha pingamizi lake sasa itazuia biashara kubwa. Lakini hiyo ndiyo bei ya kutetea uhuru wa jimbo na kidini.”
Na moja kwa moja tunaendelea na gazeti la “Märkische Allgemeine” la mjini Potsdam ambalo pia linatathmini mkutano kati ya Kansela Merkel na Dalai Lama wa Tibet. Gazeti limeandika:
“Mazumgunzo kati ya Angela Merkel na Dalai Lama hayatabadilisha hali ya Tibet, tena si tukio muhimu sana katika historia ya eneo hili. Lakini baada ya miaka mingi ya kutochukua msimamo wazi, Ujerumani imerudi kutetea sera zake kuelekea nchi za nje. China, bila shaka, ni mshirika muhimu katika biashara, lakini ikiwa Ujerumani inataka kuaminika katika kutetea haki za binadamu, inalazimika kutekeleza sera hizo dhidi ya China vilevile na huko Sudan na Urusi.”
Mhariri wa “Bonner Generalanzeiger” pia anazingatia ulinzi wa haki za binadamu akilinganisha sera za nchi mbalimbali za Ulaya. Uchambuzi wake ni kama ifuatavyo:
“Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinakaa kimya juu ya haki za binadamu. Sababu ni kwamba zinavutiwa zaidi katika uchumi wa China. Bila ya kujali haki za binadamu zinataka kufanya biashara na nchi hiyo ambayo inakuwa kwa haraka kiuchumi. Lakini nchi zenye sera kama hizo haziaminiki kuwa watetezi wa haki za binadamu katika sehemu nyingine za ulimwengu.”
Katika sifa zake kwa Kansela Merkel, mhariri wa “Ostsee-Zeitung” anakumbusha juu ya msimamo mkale wa Kansela Merkel kuhusiana na haki za bindamu:
“Viongozi wengi wa nchi nyingine wameshawahi kuona vile Angela Merkel anavyotetea sera zake: Rais Bush wa Marekani juu ya hali katika jela la Guantanamo, rais wa Poland Kaczynski kuhusu katiba ya Umoja wa Ulaya na rais Putin wa Urusi juu ya haki za binadamu.”
Na hatimaye juu ya mazungumzo kati ya Kansela Merkel wa Ujerumani na kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama ni mhariri wa “Mitteldeutsche Zeitung” ambaye anaonya kutokuwa na matumaini mengi:
“ Ni lazima kuishurutisha China juu ya haki za binadamu kabla ya michezo ya Olympiki. Lakini nchi hiyo kubwa haitakubali kubadilisha sera zake kuelekea Tibet. Kwa hivyo tunategemea kusubiri na kutumai kwamba kujifungua kiuchumi kutaleta mabadiliko ya ndani pamoja na kuwapa uhuru wananchi wa China na eneo la Tibet.”