Merkel ashindwa uchaguzi Berlin
21 Septemba 2016Sababu kuu ya chama hicho kupoteza nguvu katika uchaguzi huo wa Jumapili, ni sera ya Merkel ya kukaribisha wahamiaji. Matokeo ya jana ya chama cha CDU ni mabaya kuwahi kutokea katika jiji la Berlin, na yanamuongezea shinikizo kansela Merkel kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Chama cha CDU kimepata asilimi 17.5 ya kura zote, na kimepoteza asilimi 5.8 ya kura ikilinganishwa na uchaguzi uliopita. Huku chama mshirika cha Meya wa Berlin, Michael Müller, kinachofuata siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha SPD kikishinda asilimia 21.6 ya kura zote zilizopigwa, kikiwa kimeanguka kwa asilimi 6.7 ikilinganishwa na uchaguzi uliopita wa jimbo hilo.
Licha ya kupungua kwa uungwaji mkono wa chama chake, Meya Müller amesema chama cha SPD kimefikia lengo lake.
"Tumefikia lengo letu, bado tunasimama kama chama kilicho na nguvu zaidi katika mji huu na tuna mamlaka ya serikali. Tumewazidi washindani wetu wa asilimia 5, 6, 7. Tumefanikiwa kupata matokeo yanayo tuwezesha kuenedelea kushikilia nafasi ya umeya," amesema Müller.
Chama cha AfD kimeongeza uungwaji mkono
Wakati huo huo, chama cha mrengo wa kushoto kilichokuwa chama cha kikomunisti cha iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki, kimejiongezea asilimi 4 ya kura na kupata asilimi 15.7. Huku chama kipya cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kikishinda asilimia 14.1 ya kura zote zilizopigwa, na kujinyakuli kiti cha kumi katika uchaguzi wa majimbo.
Asilimia 66.6 ya watu walijitokeza kupiga kura, idadi hii ikiwa imeongezeka ikilinganishwa na asilimi 60.2 ya uchaguzi uliopita. Chama cha AfD kilifanikiwa kuvutia wapiga kura wapya, lakini pia kimeweza kunyakuwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya CDU na SPD pamoja na vyama vingine.
Georg Pazderski, mgombea wa chama mbadala kwa Ujerumani cha AfD amekisifu chama chake kwa namna kilivyoweza kupiga hatua katika muda mfupi tokea kuasisiwa kwake.
"Kutoka sifuri hadi tarakimu mbili, ni jambo la namna ya pekee kabisa mjini Berlin, halikuwahi kutokea kwa miaka 66. Na matokeo yanasemaje? Muungano mkuu umepoteza kura…. Bado huajapoteza kura katika kiwango cha shirikisho lakini hilo linakuja nalo mwakani," amesema Georg Pazderski.
Ingawa vyama vya Social Democratic SPD na Cristian Democratic Union CDU vimeibuka kuwa na nguvu zaidi katika uchaguzi wa jimbo la Berlin uliofanyika jana, lakini pia vimetoteza uungwaji mkono mkubwa kiasi ya kwamba havitaweza kuendelea kuongoza serikali ya muungano ya Ujerumani.
Katibu Mkuu wa chama cha CDU, Peter Tauber, ameulamu uongozi wa meya wa Berlin Müller wa muungano wa vyama vya SPD na CDU, kwa matokeo yasiyoridhisha ya chama chake cha CDU.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/ape
Mhariri: Iddi Ssessanga