Merkel ashindwa kuisaidia kijeshi Ukraine
29 Novemba 2018Angela Merkel amesisitiza uungaji mkono wa Ujerumani kwa Ukraine katika mgogoro unaoendelea kati ya nchi hiyo na Urusi, kuhusiana na meli tatu za Ukraine zilizotekwa na Urusi siku ya Jumapili, ingawa hakutishia hatua zaidi dhidi ya Urusi, iwe katika muktadha wa msaada wa kijeshi au vikwazo.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alitumia gazeti la kila siku la Ujerumani la Bild, kumuomba Merkel kutuma meli za kivita katika bahari ya Azov kutoa ulinzi, na kuituhumu Urusi kwa kutaka kuikali bahari hiyo.
Msaada wa kiuchumi, lakini hakuna uungwaji mkono wa kijeshi
Akizungumza katika mkutano wa tatu wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Ukraine leo, kansela huyo wa Ujerumani hakutoa ahadi yoyote ya moja kwa moja kuhisiana na maombi ya Poroshenko na badala yake alitilia mkazo dhamira ya Ujerumani kwa Ukraine, na kuulaumu kikamilifu mgogoro wa sasa kwa rais wa Urusi Vladmir Putin.
Amebainisha kuwa Urusi na Ukraine zilisaini mkataba kuhusu usafiri wa majini mwaka 2003, ambao unazipa nchi hizo mbili haki ya matumizi kamili ya jia ya Kerch kuelekea bahari ya Azov, ingawa pande zote pia zina haki ya ukaguzi katika bahari hiyo.
Merkel amesema daraja lililojengwa na Urusi kuelekea rasi ilioitwa kimabavu ya Crimea limezuwia uhuru wa usafiri wa meli, na kulalamika kuwa tangu kufunguliwa kwa daraja hilo mwezi Mei mwaka huu, mazingira ya usafiri wa majini yamekuwa mabaya zaidi.
Kitisho cha kupunguza manunuzi ya gesi
Amesema anataka ukweli wa yaliotokea uwekwe mezani, kuachiwa huru kwa wanajeshi wa Ukraine, na kwamba kukiri kwao kusiwe kwa kulaazimishwa, kama ilivyoonekana kwenye runinga.
Akizungumza kabla ya Merkel katika mkutano huo, waziri mkuu wa Ukraine Volodymyr Groysman amelaani kile alichokiita uvamizi wa Urusi, na kuongeza kuwa hii ni mara ya tano kwa Urusi kupuuza sheria za kimataifa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Merkel amependekeza njia moja tu ambapo Ujerumani anaweza kutumia shinikizo la ziada kwa Urusi: kwa kupendekeza kwamba mataifa ya Urusi kiwango cha gesi yanayonunua kutoka kwa Urusi kupitia mabomba yake ya Nordstream na Turkstream.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW
Mhariri: Mohammed Khelef