Merkel amuonya Trump kuhusu kuhami masoko
15 Januari 2017Marekani ni mshirika muhimu sana wa kibiashara wa Ujerumani na kauli za kuhami masoko ya biashara za rais mteule wa marekani Donald Trump zimewakera wauzaji wa nje katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika bara la Ulaya.
Ujerumani ni rais wa kundi la G20 mwaka huu linalojumuisha mataifa 20 yenye viwanda na yale yanayoinukia kiuchumi duniani, jukwaa ambalo Merkel anataka kulitumia kulinda ushirikiano wa kimataifa.
Akizungumza baada ya mkutano wa wajumbe waandamizi wa chama chake cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha CDU katika mji wa Perl-Nenning magharibi mwa Ujerumani , Merkel amesema nchi zote zitafaidika iwapo zitafanyakazi kwa pamoja badala ya kujitenga.
Mfano mzuri ulikuwa juhudi za pamoja za kimataifa baada ya mzozo wa kiuchumi duniani ambao ulianzia nchini Marekani mwaka 2008, Merkel alisema.
Juhudi za pamoja
"Jinsi mzozo wa kifedha ulivyoshughulikiwa haikuwa jibu ambalo lilikuwa katika misingi ya kujitenga, lakini lilikuwa jibu ambalo lilikuwa katika msingi wa ushirikiano, sheria za pamoja za udhibiti, ikiwa ni pamoja na masoko ya fedha," Merkel alisema.
Akiulizwa lini atakutana na Trump kwa mara ya kwanza, Merkel alisema mkutano unawezekana wakati wa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani yaani G7, ambao utafanyika Sicily mwezi Mei, na ule wa G20 utakaofanyika nchini Ujerumani mwezi Julai.
Katika hotuba yake ya kila wiki , Merkel alisema uchumi wa Ujerumani unakwenda vizuri, lakini nchi hiyo haipaswi kubweteka. Ameahimiza makampuni kuingia katika changamoto ya digitali.
"Pia kuna hatari ya kimataifa. Tunaona hatua za kuhami masoko," Merkel alisema , bila kumtaja Trump.
Viongozi wa makampuni wamesema uchumi wa Ujerumani unaweza kuathirika kutokana na sera za kibiashara za Marekani za kuhami masoko, na kwamba ukuaji wa kiuchumi unaweza kuathirika.
Uchumi wa Ujerumani umekua kwa asilimia 1.9 mwaka 2016, kasi kubwa kabisa katika miaka mitano, wakati ongezeko la matumizi ya watu binafsi na serikali vilisaidia kuimarisha nafasi yake kama injini ya ukuaji wa uchumi katika kanda ya sarafu ya euro.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Zainab Aziz