1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na viongozi wa taasisi za fedha

Sekione Kitojo7 Oktoba 2011

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekutana mjini Berlin na watu mashuhuri katika masuala ya kifedha ulimwenguni wakijadili njia za kuzisaidia benki za Ulaya zinazokabiliwa na matatizo ya kifedha

https://p.dw.com/p/12nPc
Kansela Angela Merkel amekutana na maafisa wa juu wa taasisi za fedha duniani mjini Berlin .Picha: picture alliance/dpa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekuwa mwenyeji wa mkutano mjini Berlin akikutana na watu mashuhuri katika ulimwengu wa masuala ya fedha wakijadili njia za kuzisaidia benki za Ulaya. Katika mkutano huo pia alishiriki mkuu wa shirika la fedha la kimataifa IMF Chritine Lagarde, rais anayeondoka madarakani katika benki kuu ya Ulaya, Jean-Claude Trichet na kiongozi wa benki kuu ya dunia Robert Zoellick. Merkel amesema kuwa yuko tayari kutoa msaada ili kuyaweka mabenki ambayo yanaathirika na madeni ya nchi kuweza kupata tena fedha na hatasita kuingilia kati katika masoko ya fedha iwapo itakuwa ni muhimu.

Kansela ameongeza kusema kuwa mfuko uliopanuliwa wa uokozi barani Ulaya una fedha za kutosha kuyasaidia mabenki. Hapo mapema , benki kuu ya Ulaya , ECB, iliendelea kuwa na kiwango kile kile cha riba cha asilimia 1.5. ECB pia imetangaza operesheni mbili za muda mrefu za kupata fedha kuzisaidia kifedha benki ambazo zina matatizo.