1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aionya Uingereza kuhusu soko la pamoja

6 Oktoba 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameonya kuwa Uingereza haitaweza kushiriki katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya, ikiwa itakataa kukubali sharti la uhuru wa watu kusafiri

https://p.dw.com/p/2QxyJ
Deutschland Tag der Deutschen Industrie 2016 Rede Merkel
Picha: Reuters/F. Bensch

Katika mkutano wa leo na viongozi wa sekta ya viwanda na watunga sera wa Ujerumani, Kansela Merkel ameiita kura ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya kuwa tukio la kihistoria kwa umoja huo. Amesisitiza kuwa ushiriki wa soko la pamoja la Umoja wa Ulaya utategemea na usafiri huria wa watu, la sivyo kila nchi mwanachama wa umoja huo itaanza kufanya inachotaka "Kama utaikubalia nchi moja, basi fikiria kama nchi zote zitaanza kuweka masharti yao kuhusu usafiri huria ukilinganisha na nchi nyingine zote, hili litasababisha hali ngumu kabisa.

Kansela huyo wa Ujerumani amesema kuwa mazungumzo ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya hayatakuwa rahisi. Amesema, "Hayatakuwa mazungumzo rahisi. Kuna hoja moja inayotuhusu. Kwamba sekta ya viwanda ya kila nchi itatathminiwa tofauti. Hilo ni suali la ushiriki wa soko la pamoja. Kile Uingereza inapata na kutoa, kiasi gani inaweza kushiriki na tutaingia katika soko la Uingereza chini ya masharti gani. Na namna gani tuko tayari kisiasa kushirikiana, kiasi gani cha haki za msingi kitakuwapo".

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Reuters/T. Melville

Kauli hiyo imeungwa mkono na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye hata hivyo alisema kuwa hatua hiyo haipaswi kuuzuia Umoja wa Ulaya kujaribu kuwaweka Waingereza karibu na Ulaya.

Merkel ameiahidi sekta ya kibiashara kuwa kutakuwa na mapunguzo madogo ya kodi kwa kiasi cha zaidi ya euro bilioni 6 katika mwaka wa 2017 hali ambayo pia itawanufaisha watu wa mapato ya wastani na makampuni madogo na ya wastani. Pia aliahidi uwekezaji zaidi katika sekta ya miundo mbinu ya Ujerumani kwa sababu mapato ya kodi yameongezela.

Rais wa Shirikisho la Viwanda la Ujerumani - BDI Ulrich Grillo, alikuwa na matumini kuwa Ujerumani ambayo ni nchi iliyostawi kiuchumi Ulaya itabakia katika mkondo wa ukuwaji.

Baadhi ya wanasiasa wa Uingereza wana matumaini kuwa makundi ya kiviwanda barani Ulaya, yanayohofia kupoteza nafasi za kuingia katika soko la Uingereza, yatashinikiza kuhusu mpango wa kuibakisha Uingereza katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya huku ikiudhibiti uhamiaji wa watu nchini humo.

Kauli ya Merkel imekuja siku chache tu baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kusema kuwa ataidhinisha ifikapo Machi 2017 mazungumzo ya miaka miwili ya nchi yake kutalikiana rasmi na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga